Karen Nyamu aapa kumaliza kero la vijana kufurika vilabuni Jumapili alfajiri maarufu 'Aluta'

Aluta ni njia mpya ambayo imeteka vijana wengi kujipata wakitafuta njia zako kuelekea vilabuni haswa majira ya saa kumi na moja asubuhi siku za Jumaplili kwa ajili ya kujivinjari.

Muhtasari

• Aluta huwa ni tafrija ya miziki ya Reggae iliyokolea ambayo hugeuzwa na kuwa kama ibada klabuni, walevi wakifurahia miziki hiyo hadi mwendo wa jua kuchomoza.

Karen Nyamu aluta
Karen Nyamu aluta
Image: Facebook

Seneta maalum wa kaunti ya Nairobi, Karen Nyamu amefichua kwamba katika tathmini yake ya muda, amebaini kwamba vijana wengi wamepotelea katika vilabu vya pombe na starehe.

Nyamu kupitia akaunti zake mitandaoni, alisema kwamba katika miaka ya hivi karibuni, vijana wengi wamekuwa na hulka ya kufurika vilabuni majira ya alfajiri maarufu kama ‘Aluta’ jambo ambalo linawasababisha kulewa nyakati ambazo wanastahili kurauka kwenda kazini na hivyo kuathiri pakubwa nguvu kazi ya taifa.

Nyamu aliapa kumaliza tatizo hilo akisema kwamba hiyo ni tahadhari ni kwa wamiliki wa kumbi hizo za starehe.

“Kuna kitu inaharibu vijana hapa Nairobi inaitwa ALUTA. Hio form me ndio nitaichoma. Club owners this is your notice,” Nyamu alisema.

Tafrija za Auta ni maarufu kwa vijana wengi jijini Nairobi na aghalabu hufanyika wikendi ambapo watu huanza kufurika klabuni mwendo wa saa kumi na moja asubuhi kujivinjari.

Lakini je, Aluta ni nini?

Aluta huwa ni tafrija ya miziki ya Reggae iliyokolea ambayo hugeuzwa na kuwa kama ibada klabuni, walevi wakifurahia miziki hiyo hadi mwendo wa jua kuchomoza.

Mapema saa kumi na moja asubuhi ya kila Jumapili yoyote asubuhi katika vilabu vingi Nairobi, utaona wateja wakiendelea kuifurika, DJ akiendelea kutikisa mahali hapo, wahudumu wakicheza njiani na wasichana walioloweshwa kwa mivinyi na kupotea katika kiputo cha muda cha fujo.

Na asubuhi inapokaribia, vilabu sasa vimebuni njia mpya za kuwafanya watu waendelee - Huduma ya Jumapili ya Aluta.