Ferdinand Omanyala amshukuru rais Ruto kwa kumuongezea tuzo ya kiheshima ya MBS

Omanyala mpaka sasa ndiye mshikilizi wa rekodi ya mbio za mita 100 kutoka bara la Afrika na pia ndiye mshindi wa mashindano ya Commonwealth.

Muhtasari

• "Asante Mheshimiwa Rais,” Omanyala aliandika akiambatanisha picha yake akisalimiana na rais Ruto.

 

Ferdinand Omanyala
Ferdinand Omanyala
Image: Facebook

Mwanariadha wa mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala amevuja kimya chake baada ya rais Ruto kumtunuku kwa tuzo nyingine ya kiheshima.

Omanyala alikuwa miongoni mwa Wakenya wengi ambao walipongezwa kwa kazi zao nzuri katika mwaka huu wa 2023 katika Nyanja mbalimbali.

Rais Ruto katika hotuba yake ya siku ya Jamhuri kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Kenya, alimtunuku Omanyala tuzo ya kiheshima ya Moran of the Order of the Burning Spear, MBS miongoni mwa wanariadha wengine.

Hii ni tuzo ya pili ya kiheshima kwa Omanyala kutoka kwa mkuu wa nchi baada ya kupewa ile ya Order of the Grand Warrior of Kenya, OGW mwaka 2021 na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Ilianza The Order of the Grand Warrior (O.G.W) sasa imeongezwa Moran of the Order of the Burning Spear (M.B.S.) kwenye jina langu. Asante Mheshimiwa Rais,” Omanyala aliandika akiambatanisha picha yake akisalimiana na rais Ruto.

Mwanariadha huyo aliibuka ghafla kwenye ndimi za wapenzi wa riadha Kenya mwaka 2021 baada ya kufana katika mashindano ya Olimpiki jijini Tokyo Japan alikoweka rekodi nzuri kwa mbio za mita 100 kutoka Afrika lakini kwa bahati mbaya hakuweza kushinda dhahabu.

Omanyala mpaka sasa ndiye mshikilizi wa rekodi ya mbio za mita 100 kutoka bara la Afrika na pia ndiye mshindi wa mashindano ya Commonwealth.