Mulamwah: Nyumba yangu mpaka kukamilika itakuwa imenigharimu milioni 15

“Ni kitu ambacho kinawezekana, tu asikuambie kwamba huwezi, ni kujipanga tu na kujiambia kwamba unajua nini inawezekana na unajitoa kimasomaso kuifanya, rahisi tu hivyo." alisema.

Muhtasari

• Mchekeshaji huyo ambaye ni baba mtarajiwa amekuwa akiwatembeza mashabiki wake kwa safari ya ujenzi wa mjengo huo ambao ni muundo wa ghrofa.

Mulamwah
Image: Facebook

Mchekeshaji Mulamwah amefichua kiasi cha hela ambazo mjengo wake wa kifahari nyumbani kwao kijijini katika kaunti ya Trans Nzoia itamgharimu mpaka kukamilika kabisa.

Mulamwah alianza mjengo huo mwaka jana miezi michache baada ya kuachana na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonie.

Mchekeshaji huyo ambaye ni baba mtarajiwa amekuwa akiwatembeza mashabiki wake kwa safari ya ujenzi wa mjengo huo ambao ni muundo wa ghrofa.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni siku mbili zilizopita katika uzinduzi wa filamu ya mchekeshaji mwenza, Terence Creative, Mulamwah alifichua kwamba japo wengi wanaona ni rahisi, kwa upande wake haijakuwa rahisi kusimamisha mjengo wenye haiba kama ile.

Alisema kwamba kuanzia msingi hado pahali imefikia nyumba hiyo, amekuwa akitegemea pesa zake pekee bila mkopo wowote na kufichua kwamba mpaka kukamilika kwake, itakuwa imemgharimu kiasi kisichopungu shilingi za Kenya milioni 15.

“Safari imekuwa ngumu, ni kujinyima kwa sababu hakuna kitu rahisi. Hata ukisema unataka kununua koti kesho lazima utaruka chakula cha mchana kama mara mbili tatu hivi, yote ni kutokana na kujitolea, kujinyima na kutia bidii. Lazima hizo pesa utafute kwa sababu pale hakuna mtu atakupa mkopo, ni hela yako taslimu kwa hiyo utakuwa hulali, unazunguka kuzitafuta…” alisema.

“Ni kitu ambacho kinawezekana, tu asikuambie kwamba huwezi, ni kujipanga tu na kujiambia kwamba unajua nini inawezekana na unajitoa kimasomaso kuifanya, rahisi tu hivyo. Mpaka wakati namalizia ni pesa poa, haiwezi kuwa chini ya milioni 15 hivi,” aliongeza.