"Nilifeli KCSE lakini nilifanya safari 45 za kigeni mwaka jana kwa nchi 27" - Larry Madowo

Aliwataka vijana wanaoambiwa kuwa walifeli kutowasikiliza wasemaji wa maneno hayo kwao hatima ya mja I mikononi mwa Mungu tu wala si kwenye midomo ya walimwengu.

Muhtasari

• Miongoni mwa nchi ambazo Larry ametembelea ni Misri, Uswizi, Ureno, Morocco, Nepal, Rwanda, Norway, Nigeria, Marekani, Tanzania, Uholanzi, Afrika Kusini miongoni mwa nchi nyingine.

Larry Madowo,
Larry Madowo,
Image: X

Mwanahabari wa CNN Larry Madowo amefichua kwamba ‘alifeli’ mtihani wake wa mwisho katika shule ya sekondari, KCSE lakini hakufa moyo mpaka akaja kuwa Larry Madowo wa sasa.

Kupitia kurasa zake za mitandaoni, Larry aliweka ujumbe huo kama njia moja ya kuwatia moyo vijana ambao walifanya KCSE mwaka jana na matokeo yao kutangazwa rasmi Jumatatu Janauri 8 na waziri wa elimu Ezekiel Machogu.

Larry alisema licha ya wazazi wake kumtaka kurudia kidato cha nne kwa sababu ya ‘kufeli’ lakino leo hii anasimama kama kielelezo kizuri na mtu ambaye wengi wanamtazamia kama mfano bora katika jamii na kwenye taaluma ya uanahabari.

Madowo alijitapa kuwa kwa mwaka wa 2023 pekee, alifanya ziara zipatazo 45 katika mataifa 27 tofauti, na hiyo inaonyesha jinsi amefanikiwa pakubwa kimaisha.

Aliwataka vijana wanaoambiwa kuwa walifeli kutowasikiliza wasemaji wa maneno hayo kwao hatima ya mja I mikononi mwa Mungu tu wala si kwenye midomo ya walimwengu.

““Nilifeli” KCSE lakini nilifanya safari 45 za kigeni mwaka jana - nchi 27. B- yangu katika mtihani wa kitaifa ilikuwa mbaya sana nikasukumwa kurudia kidato cha 4! Mtu asikupimie hewa,” Larry Madowo alisema.

Miongoni mwa nchi ambazo Larry ametembelea ni Misri, Uswizi, Ureno, Morocco, Nepal, Rwanda, Norway, Nigeria, Marekani, Tanzania, Uholanzi, Afrika Kusini miongoni mwa nchi nyingine.

Akitangaza matokeo ya KCSE Jumatatu kutoka shule ya upili ya wasichana ya Moi mjini Eldoret, waziri Machogu alionyesha kutikitishwa kwake na idadi kubwa ya watahiniwa ambao walizoa alama za E.

“Nimeumizwa na ukweli kwamba idadi kubwa ya watahiniwa (48,174 au 5.33%) bado waliishia kupata alama 38 za wastani za E katika Mtihani wa KCSE wa 2023 hata baada ya Wizara kutumia mfumo rahisi zaidi wa kukokotoa matokeo ya mwisho ya watahiniwa,” alisema.

Rais Ruto pia alitaka wizara ya elimu kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini kiini cha idadi hiyo kubwa ya wanafunzi waliofeli.