Karen Nyamu atafuta wasichana 11 wenye uhitaji ili kufadhili masomo yao ya sekondari

“Kwa zaidi ya Miaka 30 ya Ubora wa Kiakademia, na Uwezeshaji wa Mtoto wa Kike, Muundo wa ada unaopatikana kwenye google ada za kusoma zaidi ya 100k kwa muhula,” Nyamu alibaini.

Muhtasari

• Ili kuhitimu, wasichana lazima wawe wahitimu wa juu kimasomo waliopata alama 400 na zaidi katika KCPE

Wanafunzi wakiwa kwenye maabara.
Wanafunzi wakiwa kwenye maabara.
Image: Facebook//KarenNyamu

Seneta maalum Karen Nyamu ametangaza nia ya wakfu wake kutafuta wasichana angalau 11 wenye uhitaji wa kipekee kwa ajili ya kufadhili masomo yao ya shule ya upili.

Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, Nyamu kupitia kwa wakfu wake wa Karen Nyamu Foundation, alisema wameshirikiana na shule ya upili ya wasichana ya St. Lucie Kiriri ili kufanikisha ndoto za wasichana 11 wanaohitaji msaada wa kimasomo kuanzia Januari hii.

Katika nafasi hizo, Nyamu alisema anahitaji wasichana 4 wanaotaka kujiunga kidato cha kwanza na 7 ambao wanataka kujiunga kidato cha 3.

“Karen Nyamu Foundation imeshirikiana na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Lucie Kiriri kudhamini kikamilifu wasichana 4 wa uandikishaji wa kidato cha kwanza na uandikishaji wa 7 wa kidato cha 3,” Nyamu alisema.

Lakini je, ni vipi mtu anaweza kupata fursa hizo na vigezo ni vipi?

“Ili kuhitimu, wasichana lazima wawe wahitimu wa juu kimasomo waliopata alama 400 na zaidi katika KCPE. Lazima awe kutoka kaunti ya Nairobi (au aonyeshe uhitaji mkubwa ikiwa anatoka kaunti tofauti) na awe mtoto mwenye uhitaji.”

“Kwa udahili wa kidato cha 3, lazima uwe umefunga B+ katika mitihani yako ya hivi punde ya kidato cha 2 au umepata zaidi ya alama 400 katika KCPE yako,” aliongeza.

Shule hiyo ni ya kibinafsi ambayo imekuwa humu nchini kwa Zaidi ya miaka 10 na Nyamu alifichua kuwa gharama yake ya karo kwa kila muhula ni Zaidi ya laki moja.

“Kwa zaidi ya Miaka 30 ya Ubora wa Kiakademia, na Uwezeshaji wa Mtoto wa Kike, Muundo wa ada unaopatikana kwenye google ada za kusoma zaidi ya 100k kwa muhula,” Nyamu alibaini.