Robert Burale adai ana mbwa German Shepherd karibia 8 wa kumlinda bintiye

Baadhi ya watu walimtania kwamba bintiye ameshakuwa mkubwa na ndio ule wakati mzazi anaanza kuhangaika na kumlinda binti kutokana na majaribu ya vijana wa hovyo.

Muhtasari

• “Uzuri wa maisha ni kujua urithi wako uko salama katika Kristo,” Burale aliambatanisha kwenye picha na bintiye.

ROBERT BURALE NA BINTIYE
ROBERT BURALE NA BINTIYE
Image: Facebook

Robert Burale amefichua kwamba ana mbwa aina ya German Shepherd karibia wanane ambao ni mahususi kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa bintiye tineja.

Mhubiri huyo ambaye pia ni mtoa nasaha alifichua haya kupitia ukurasa wake wa Facebook alipokuwa anamjibu mtumizi mmoja wa mtandao huo aliyetoa maoni kwenye chapisho lake.

Burale alichapisha picha ya pamoja akiwa na bintiye mkubwa na kusema kwamba kinachompendezesha Zaidi na maisha yake na bintiye ni kuwa na uhakika kwamba Mungu ndiye yuko kwenye usukani wa maisha yao.

“Uzuri wa maisha ni kujua urithi wako uko salama katika Kristo,” Burale aliambatanisha kwenye picha na bintiye.

Watu walitoa maoni wakisema kuwa binti huyo ameshakuwa mtu mzima haraka sana na wengine wakidai kwamba tunda halijadondoka mbali na mti, kwa maana ya kulandana kama shilingi kwa ya pili na babake.

Mwingine alimwambia kuwa kwa vile ameshakuwa mkubwa sasa, anahitaji ulinzi mkali ili asije akachezewa na vijana wa hovyo, na kumuuliza Burale kwa njia ya utani iwapo aejipanga kwa ajili ya kibarua hicho kigumu cha kumlinda msichana tineja.

“Lo! . yeye si msichana mdogo tena! Wako wapi mbwa German Shepherd wa kumlinda. . hahaaa!” Obed King Musumbi alimuuliza kwa utani.

Burale alimjibu kwamba mbwa hao wako kabisa kwa ajili ya ulinzi wa binti yake na hata kutoa maelezo ya kina Zaidi kuhusu idadi ya walinzi wa bintiye.

“Wako kabisa… karibia 8 hivi,” Burale alijibu kwa utani.

Burale
Burale