KRG atoa ombi la kipekee kwa Wakenya, ataka kusaidiwa kwa mwaka mmoja tu!

“Mimi nimejuana na Konshens kitambo, kupitia kwa produsa mwingine anaitwa Damien Gelle ambaye nilimleta Kenya 2017. Ni vile sikuwa nataka kufanya muziki mimi" KRG alisema.

Muhtasari

• Msanii huyo aidha alijitapa kwamba yeye ataibadilisha sura ya muziki wa Kenya peke yake kama jeshi la mtu mmoja.

KRG
KRG
Image: Facebook

Msanii KRG the Don ametoa ombi la kipekee kwa Wakenya kipindi hiki ambapo anavuma kote mitandaoni kufuatia ngoma yake mpya aliyomshirikisha msanii wa Jamaika, Konshens.

Akizungumza katika mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio humu nchini, KRG alisema kwamba anataka Wakenya kuwa nyuma yake kwa kipindi cha mwaka mmoja tu ilikuwaletea matunda ya muziki ambayo wamekuwa wakiyaona kwa wasanii wa mataifa jirani.

“Sasa hivi kile kitu kimoja ambacho kimebaki, naomba tu kitu kimoja kwa Wakenya, mnisapoti tu, sitaki sapoti ya muda mrefu, mwaka mmoja tu, mwaka huu tu ili niwabadilishie hii landscape ya muziki wa Kenya niibadilishe kabisa,” KRG aliomba.

Msanii huyo aidha alijitapa kwamba yeye ataibadilisha sura ya muziki wa Kenya peke yake kama jeshi la mtu mmoja.

“Sitaki msanii mwingine yeyote wa nyumbani alisapoti, ni mashabiki tu.”

Msanii huyo kwa undani aliweza kuelezea ni nini hicho ambacho anataka kukibadilisha kaitka sura ya muziki wa Kenya.

“Kwanza nataka kuvunja hiyo laana kwamba kuna kiwango Fulani ambacho muziki wa Kenya huwezi kufika, nataka isahaulike kabisa na kuhakikisha kwamba msanii wa Kenya anawza kufika ughaibuni kutoka huku nyumbani, yaani ile wewe uko hapa nyumbani lakini unachukua pesa kutoka nchi kama Marekani, sio hizi shoo unaitwa kwa kundi la Wakenya hapana,” alisema.

“Nataka ukienda Marekani lazima Wamarekani wakusikilize, vile wanamheshimu Burna Boy na Wizkid nataka waheshimu kila msanii kutoka sehemu yoyote aiwemo Bughaa. Nikipata tu sapoti ya Wakenya kidogo tu, nitawarushia madini na mabomu kutoka hapa yatingize dunia mzima, kutoka hapa Kenya tu,” aliongeza.

Msanii huyo alisema kwamba aliunganishwa na Konshens na produsa Fulani mwaka 2017 akisema kwamba angetaka kuanza kufanya muziki kipindi hicho angeanza lakini ni vile alikuwa ameshikika kidogo na masuala yake ya kibiashara.

“Mimi nimejuana na Konshens kitambo, kupitia kwa produsa mwingine anaitwa Damien Gelle ambaye nilimleta Kenya 2017. Ni vile sikuwa nataka kufanya muziki mimi, nyinyi mnajua mimi nilikuwa tu mmiliki wa lebo, wasanii wangu wote wameshatusua kwa hiyo nikasema sasa wale washakuwa watu wazima, wacha pia mimi niwaonyeshe ninaweza fanya hii kitu,” alisema.