Dvoice asimulia jinsi maisha yake yalivyobadilika ghafla baada ya kusainiwa na Diamond WCB

“Kusema kweli kwa mara ya kwanza ilikuwa ni ngumu sana. Sema sasa hivi nimeanza kuzoea kuwa na mabaunsa" alisema Dvoice,

Muhtasari

• “Yaani nilikuwa nashangaa kinachowafanya wanilinde wanalinda nini maana sina kitu ninachomiliki cha kuwafanya watu labda wakatamani kuniua." alisema.

DVOICE
DVOICE
Image: Screengrab//WasafiMedia

Miezi miwili baada ya msanii Dvoice kusainiwa ndani ya lebo ya WCB Wasafi inayomilikiwa na mbabe Diamond Platnumz, msanii huyo amepiga kisengerenyuma jinsi alilazimika kubadili baadhi ya vitu ambavyo alikuwa anavizoea katika maisha yake ya kawaida.

Dvoice ambaye alikuwa anazungumza kwenye kituo cha Wasafi FM alisema kwamba pindi baada ya kusainiwa, alilazimika kuacha kufanya baadhi ya vitu lakini pia tukio kubwa lililomshangaza ni pale alipokabidhiwa walinzi kwa maana ya mabaunsa kumpa ulinzi muda wote kokote aendako.

Kinda huyo mkali wa tungo za Singeli alisema kwamba mwanzoni alikuwa anashangaa mbona analindwa na mabaunsa muda wote kwa sababu aliona hakuwa na chochote cha kuweza kuporwa lakini kadri muda ulivyozidi kusonga, aielewa ni kwa nini.

“Kusema kweli kwa mara ya kwanza ilikuwa ni ngumu sana. Sema sasa hivi nimeanza kuzoea kuwa na mabaunsa. Kuna kipindi nilikuwa nawaambia eeh bwana ndugu zangu eh... kwa sababu nilikuwa sioni cha kunilinda, nilikuwa nashangaa wananilinda nini?” Dvoice alisema.

“Yaani nilikuwa nashangaa kinachowafanya wanilinde wanalinda nini maana sina kitu ninachomiliki cha kuwafanya watu labda wakatamani kuniua. Lakini ilifika mahali nikatambua thamani yangu, jinsi watu wanavyoniitikia unapita mahali unapata watu wanakuchangamkia kutaka kukukumbatia kumbe labda wana visu, kwa hiyo mabaunsa wanasaidia,” aliongeza.

Msanii huyo mpaka sasa ana miezi miwili kama msanii wa WCB lakini baadhi ya wachambuzi wa Sanaa wanahisi kwamba hajatusia kihivyo.

Wengi wanasema kwamba ngoma zake ambazo zimeingia mjini ni zile alizoshirikishwa na wasanii wakubwa kwenye lebo akiwemo Zuchu na Lava Lava lakini ngoma zake za kujisimamia bado hazijapata mapokezi makubwa kwenye soko.

Dvoice alisainiwa na kuonekana kuwa mbadala wa kuziba pengo lililoachwa na Rayvanny aliyetimka na kuanzisha lebo yake mapema mwaka 2022.