Haji Manara kujaza wageni 50k uwanja wa kitaifa kwa ajili ya sherehe ya harusi yake

Mwanamume huyo wa kujilewesha kwa sifa alifichua kwamba wageni wapatao elfu 50 wataujaza uwanja huo wa kitaifa ambao umeshapitishwa tayari na CAF kuandaa michuano ya Afcon mwaka 2027

Muhtasari

• Licha ya kukashifiwa kwa kumchukua mke wa mtu na kumfanya kuwa mkewe, Manara amekuwa akiyatia masikio yake nta asiweze kusikia ushauri wa aina yoyote.

HARUSI
HAJI MANARA NA MKEWE ZAYLISSA// HARUSI
Image: FACEBOOK

Aliyekuwa msemaji wa mpira katika timu za soka za Simba SC na Yanga nchini Tanzania, Haji Manara ametangaza ujo mkubwa wa sherehe ya harusi yake na mkewe mpya, muigizaji Zaylissa.

Manara kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, alithibitisha hilo akisema kwamba wengi wamekuwa wakimuuliza kuhusu ukubwa wa tukio hilo utakuwa kiasi gani kama tukio dogo la kuvishana pete lilikuwa kubwa kiasi kile wiki mbili zilizopita.

 Manara alijibi akisema kwamba ni kweli tukio la sherehe ya harusi yake litasimamisha mitaa yote kwani siku hiyo kila barabara itakuwa inaelekea katika uwanja wa kitaifa wa Benjamin Mkapa kushuhudia tukio lake na barafu wa moyo wake.

"Naulizwa sana kuhusu sherehe ya Harusi, itafanyika au itakuwaje? Je mtaifanya kwa ukubwa gani kama Engagement Party tu ilikuwa Royal! Ndio, Tutafanya InshaAllah na itakuwa katika Standard kubwa kuzidi ya juzi na tushaanza mazungumzo ya kina kupata Tv rights na Vituo vya Television nchini,” Manara alisema.

Mwanamume huyo wa kujipata na kujilewesha kwa sifa alifichua kwamba wageni wapatao elfu 50 wataujaza uwanja huo wa kitaifa ambao umeshapitishwa tayari na CAF kuandaa michuano ya Afcon mwaka 2027.

"Itaitwa LE GRAND ROYAL WEDDING PARTY na tunakusudia kuifanyia Benjamin Mkapa Memorial Stadium, tukitazamia wageni Elfu HAMSINI kuhudhuria!! Tutaipamba ile stadium kisawa sawa na haitajulikana kabisa kama ni uwanja wa Mpira,” aliongeza.

Licha ya kukashifiwa kwa kumchukua mke wa mtu na kumfanya kuwa mkewe, Manara amekuwa akiyatia masikio yake nta asiweze kusikia ushauri wa aina yoyote kwani ikishapenda roho tena, mlo ni nyama mbichi tu!

Itakumbukwa Zaylissa, ambaye ni mke mpya wa Manara alikuwa ni mke wa msanii wa Singeli Dulla Makabila.

Dulla baada ya kugundua mkewe amevuka mstari na kwenda upande wa pili, alionesha kusikitishwa kwake na kwa uchungu akaingia studioni na kuwatungia wimbo wa kuwachamba wapenzi hao wapya lakini pia wasanii wenza waliotokea katika tafrija ya kuvishana pete kwao akisema kwamba ni wambea na wanafiki.