Msanii wa Gengetone na Mugithi Miracle Baby afanyiwa upasuaji wa 3 ndani ya mwezi mmoja

Miracle Baby alifanyiwa upasuaji wa kwanza Januari 18 kwa kile ambacho mpenzi wake Carol Katrue alifichua kwamba kulikuwa na tatizo katika utumbo wake.

Muhtasari

• Mhisani Karagu Muraya aliongoza umati unaomfuata kumchangishia Miracle Baby kiasi cha milioni moja kwa ajili ya matibabu yake.

Miracle Baby
Miracle Baby
Image: Instagram

Mwanamuziki wa Gengetone na Mugithi Peter Mwangi almaarufu Miracle Baby amefanyiwa upasuaji wa tatu Jumanne alasiri, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mpenzi wake Carol Katrue.

Katrue alithibitisha hili kwa mashabiki wao kupitia Instagram yao Jumanne akisema kwamba mpenzi wake alikuwa anaratibiwa kufanyiwa upasuaji wa tatu na kuwataka mashabiki kumweka katika maombi.

“Anaenda kufanyiwa upasuaji wa tatu, tunahitaji maombi yenu jamani,” Katrue aliandika kwenye picha ya Miracle Baby akiwa amenyong’onyea na kuonekana kukosa matumaini.

Mnamo Alhamisi, Januari 18, 2024, Carol Katrue alichapisha picha inayoonyesha mpenzi wake, akiwa amevaa barakoa ya oksijeni, akiwa amepumzika kwenye kitanda cha hospitali.

miracle baby,
miracle baby,

Hata hivyo, Katrue alichagua kutotoa taarifa za kina kuhusu hali ya Miracle Baby, badala yake alitangaza tu kwamba baba ya mtoto wake alikuwa amefanyiwa upasuaji uliofaulu.

Mama wa mtoto mmoja pia aliwaomba mashabiki wake maombi.

"Asante Mungu kwa upasuaji uliofaulu lakini endelea kumuombea," Carol Katrue aliandika kwenye InstaStories.

Katika ujumbe huo, Katrue alieleza kuwa babake mtoto wake alifanyiwa upasuaji kutokana na kupasuka kwa utumbo.

Alitaja kwamba mwanamuziki huyo angehitaji kutumia mrija kwenda chooni kwa muda wa wiki sita kwa sababu sehemu ya utumbo wake ilikuwa imetoka nje ya mwili wake.

Mama wa mtoto mmoja alisema kwamba Miracle Baby angehitaji kufanyiwa upasuaji mwingine katika siku zijazo ili kuweka matumbo yake mengine ndani ya mwili wake.

“Habari zenu, jamani upasuaji ulifanikiwa lakini utumbo ulikuwa umepasuka na wamefanikiwa kuosha lakini atakuwa anaenda chooni kupitia bomba na wameacha utumbo nje kwa muda wa wiki 6 na akipona atarudi theatre. ili matumbo yarudishwe ndani," Carol Katrue aliandika.

Itakumbukwa pia siku chache zilizopita taarifa zilitoka kwamba msanii huyo alikuwa anahitaji msaada wa angalau shilingi milioni moja kufanikisha matibabu yake.

Mhisani Karagu Muraya aliongoza umati unaomfuata kumchangishia Miracle Baby kiasi cha milioni moja kwa ajili ya matibabu yake.