Ushauri wa Manzi wa Kibera kwa Miracle Baby baada ya kutumia bili ya 88K klabuni

Manzi wa Kibera alitabiri kuwa Miracle Baby atakuja kuanza kulia tena mitandaoni akiitisha msaada lakini kwa bahati mbaya ameshawaonesha Wakenya jinsi anatumia pesa zake.

Muhtasari

• "Mimi ningepata nafasi ya pesa hizo naziwekeza kwa miradi ya maana kwa mustakabali wangu,” Manzi wa Kibera alisema.

Carol Katrue atangaza kuwa singo
Carol Katrue atangaza kuwa singo
Image: Instagram

Siku moja baada ya aliyekuwa msanii wa Gengetone Peter Miracle Baby kupakia risiti akijitapa jinsi alitumia bili ya takribani laki moja kujivinjari tu klabuni, mwanasosholaiti Manzi wa Kibera amempa ushauri.

Mpenzi wa Miracle Baby, Carol Katrue alipakia risiti hiyo ikionesha bili ya vyakula na vinywaji ghali walivyovitumia kwenye klabu kwa usiku mmoja, ikiwa Zaidi ya elfu 87 pesa za Kenya.

Hata hivyo, baadhi ya wanamitandao walihisi ni mchezo wa kughushi ili kuwaaminisha watu kuwa wako vizuri upande wa hela.

Lakini kwake Manzi wa Kibera ambaye anatoka kimapenzi na mzee wa miaka 66, anachokifanya Miracle Baby kitakuja kumponza baadae akifilisika na kuhitaji msaada wa hela kutoka kwa watu, kwani watamkumbusha jinsi alivyokuwa anazitapakaza hela zake kwa starehe.

Manzi wa Kibera alimshauri kuwa anafaa kutafuta vitu vya muhimu kuwekeza pesa zake kuliko kuzitumia kwa starehe ya muda mfupi, huku yeye akisema angepata mtu wa kumpa pesa angeziwekeza kwa miradi ya maana.

“Wekeza pesa zako, kesho utaanza kulia kwa YouTube. Lakini angalau watu mmeona vitu vya kipuuzi ambavyo maceleb wenu wanafanya na baadae wanaanza kulia. Mimi ningepata nafasi ya pesa hizo naziwekeza kwa miradi ya maana kwa mustakabali wangu,” Manzi wa Kibera alisema.

Katrue katika picha hiyo ya skrini alimtania Miracle Baby akisema kuwa hajali kama wako na mtoto.

Miracle Baby alivuma kati ya mwaka 2019 na 2021 kwa miziki ya gengetone lakini mambo yalilisakama kundi lao la Sailors Gang pale ambapo aliyekuwa meneja wao alichukua kila kitu na kuondoa ufadhili.

Msanii huyo baadae aliipata nyota yake katika muziki wa Mugithi ambao wamekuwa wakifanya na mpenzi wake Carol Katrue.