Director Trevor amtakia Mungai Eve mazuri katika chaneli yake mpya baada ya kumfuta kazi

Mungai Eve ameamua kujikusanya na kujikung’uta mavumbi baada ya kutupwa chini na Trevor kutoka kwa chaneli ambayo waliikuza pamoja.

Muhtasari

• Trevor pindi alipofikiwa na taarifa hizi, alimtakia Mungai Eve mazuri katika safari yake ya kijasiri akisema kwamba hana kinyongo naye licha ya kumfukuza kazi.

Trevor amtakia mema Eve
Trevor amtakia mema Eve
Image: Instagram

Mwanzilishi wa chaneli ya Kenya Online Media, awali ikiitwa Mungai Eve Media, Director Trevor amevunja kimya chake baada ya kupata taarifa kwamba mrembo huyo ameanzisha chaneli yake ya YouTube baada ya kumfuta kazi siku chache zilizopita.

Mungai Eve alifichua taarifa njema kwa mashabiki wake kupitia Instagram kwamba ameamua kujikusanya na kujikung’uta mavumbi baada ya kutupwa chini na Trevor kutoka kwa chaneli ambayo waliikuza pamoja.

Mrembo huyo alisema amefungua chaneli yake mpya na kuwataka kumfuata kwa sapoti kama ambavyo wamekuwa wakimuasa tangu Trevor alipotangaza kwamba huduma zake kwenye chaneli yao ya pamoja hazihitajiki tena.

Trevor pindi alipofikiwa na taarifa hizi, alimtakia Mungai Eve mazuri katika safari yake ya kijasiri akisema kwamba hana kinyongo naye licha ya kumfukuza kazi.

“Sisi kutoka Kenya Online Media tunamtakia Mungai Eve kila la kheri katika safari yake mpya,” Trevor aliandika kwenye instastory akiambatanisha na tangazo la Mungai Eve.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Mungai kugusia suala la kufukuzwa katika chaneli ya zamani baada ya kurejea nchini kimya kimya kutoa ziara ya kujivinjari kisiwani Zanzibar iliyochukua takribani wiki moja.