Magix Enga azungumzia madai ya kuwatapeli wasanii chipukizi kipindi akiwa produsa tajika

"Hapo hata ndio depression ilianzia juu walikuwa wanapeana namba yangu baada ya kuwaibia kwa kutumia namba zao,” alisema.

Muhtasari

• Msanii huyo alisema kwamba kuna kipindi hadi alipokea malalamishi kwamba ukurasa wake umemtapeli msanii chipukizi na kumhadaa kumtumia gari kumbe si kweli.

Magix Enga
Magix Enga
Image: Facebook,

Produsa na msanii anayetajwa kuwa mwanzilishi wa mdundo wa Gengetone, Magix Enga kwa mara ya kwanza amezungumzia madai yanayoendelezwa mitandaoni kwa muda mrefu kwamba utapeli ndicho chanzo kikubwa kilididimiza jina lake.

Akizungumza kwenye podikasti ya Mseto East Africa, Magix Enga alisema kwamba madai hayo si kweli.

Hata hivyo, Enga alikiri kwamba utapeli unaozungumziwa ulikuwa unaendeshwa kupitia ukurasa wake wa Facebook ambao kipindi hicho ulidukuliwa bila yeye kujua.

Mzalishaji huyo ambaye kwa sasa anafanya kazi kwenye studio ya kurekodi mziki mjini Eldoret alisema kwamba watapeli walikuwa wanasubiri ameweka tangazo la kurekodi ngoma na mbaya ya simu ya kumfikia, halafu wao wanaingia na kuhariri namba na kubadilisha na yao kisha kuanza kuwatapeli wanaotaka kurekodiwa ngoma.

“Kuna wakati ukurasa wangu wa kwanza Facebook ulikuwa na wafuasi 150k, kisha ikakua hadi kufikisha wafuasi 200k, haikuwa bado imethibitishwa rasmi lakini ilidukuliwa. Hawa watapeli walikuwa wajanja, sikujua kama imedukuliwa kipindi hicho. Nilikuwa nikiweka namba, wanaingia wanaibadilisha na kuweka yao, kisha wanaanza kuwatapeli watu, waliendelea hivyo mpaka wakaniondoa kabisa na kuichukua,” Enga alisema.

Msanii huyo alisema kwamba kuna kipindi hadi alipokea malalamishi kwamba ukurasa wake umemtapeli msanii chipukizi na kumhadaa kumtumia gari kumbe si kweli.

“Walikuwa wanatoza watu, wanawambia ni aje, hata nitakutumia gari ikuchukue ikupeleke studio, wewe tuma pesa. Halafu ni wajanja walikuwa hadi wanatumia video zangu za Instagram. Walihadaa watu wengi, na huyo hakuwa mimi. Zilikuwa namba nyingi niliziandika karibu kama kurasa tatu za kitabu,” aliongeza.

“Wengi niliwaambia waende wakapige ripoti, hiyo kesi hata nilikuwa nimeipeleka kituo cha polisi Kasarani hapo kwa ofisi ya DCI, nyingine pia niliweka Nakuru. Wale walitapeliwa nawaambia pole. Hapo hata ndio depression ilianzia juu walikuwa wanapeana namba yangu baada ya kuwaibia kwa kutumia namba zao,” alisema.