Lulu: Kuvaa vazi refu kunanipa heshima zaidi, lakini simaanishi nguo fupi ni kukosa heshima!

"Na sisemi eti nguo fupi ni kukosa heshima, hapana. Yaani ni kila mtu na starehe zake, mimi starehe yangu ni kwa nguo fupi,” Lulu Hassan alisema.

Muhtasari

• Kwa maneno yake, Lulu alisema kwamba ili ndoa kudumu, lazima kuwe kwanza na urafiki na heshima kisha mapenzi na virutubishi vingine vije baadae.

LULU HASSAN
LULU HASSAN
Image: Facebook

Mwanahabari Lulu Hassan amezungumzia kadhia ya chaguo la mavazi kwa mwanamke na uhusiano wake na muda wa kudumu kwenye ndoa.

Akizungumza na SPM Buzz, Lulu Hassan alisisitiza kwamba chaguo la vazi halina uhusiano wowote na kudumu au kubuma kwa ndoa lakini pia akasisitiza kwamba hakuna chuo kinachofunza kuhusu ndoa.

Lulu alisema kwamba ili ndoa kudumu, kwanza lazima kuwe na kujitolea kwa mtu, na wala si kuiga kile ambacho wengine wanafanya.

Lakini pia akijizungumzia mwenyewe kuhusu chaguo lake la mavazi marefu muda wote, Lulu alisema kwamba ni kupenda kwake kwani hiyo ndio njiia ya kujizolea heshima hata Zaidi.

Hata hivyo, mwanahabari huyo alisema kwamba hilo halina maana kwamba wanawake wanaochagua mavazi mafupi hawapewi heshima.

“Mimi ni kupenda kwangu na nikivaa hivi Napata heshima Zaidi. Ni jinsi ambavyo mtu anajibeba ndio chapa kubwa kubwa zinataka kuwa mwambata wako kibiashara. Na sisemi eti nguo fupi ni kukosa heshima, hapana. Yaani ni kila mtu na starehe zake, mimi starehe yangu ni kwa nguo fupi,” Lulu Hassan alisema.

Lulu alidokeza siri katika ndoa yake kudumu kwa muda mrefu ni kuelewana na mumewe Rashid Abdallah lakini pia kuwa marafiki wakubwa kabla ya mapenzi.

Kwa maneno yake, Lulu alisema kwamba ili ndoa kudumu, lazima kuwe kwanza na urafiki na heshima kisha mapenzi na virutubishi vingine vije baadae.

Lulu alifichua kwamba yeye hamuiti Rashid kama ‘mume wangu’ bali anamchukulia kama rafiki yake wa karibu na kusema tangia Rashid ajiunge na shirika la habari la Royal Media Services, wamekuwa wakiongozana kutoka na kurudi nyumbani muda wote.