Nyota Ndogo ajitolea kumrudisha Stevo Simple Boy shuleni ili kupata elimu ya kusoma na kuandika

“Tulipokutana naye kwenye ile show Nairobi nilimuangalia nikamuhurumia sana sababu alikuwa ni kama mtu anayeendeshwa. Yaani anakuwa anacontroliwa. Fanya hivi fanya vile.” Nyota Ndogo alikumbuka.

Muhtasari

• Pia msanii huyo alitoa sababu zake kuu kwa nini analenga kwa kumfadhili kimasomo na si kumsaidia kutoboa kimuziki.

• “Huyu kijana asipopata usaidizi basi maisha yake yatapotea hivi hivi mkiona. Kwaufupi nahisi anateseka sana," Nyota Ndogo alisema.

Nyota Ndogo ajitolea kumpeleka shuleni Stevo Simple Boy
Nyota Ndogo ajitolea kumpeleka shuleni Stevo Simple Boy
Image: FACEBOOK

Msanii Nyota Ndogo kutoka kaunti ya Taita Taveta amejitolea kuifadhili upya safari ya elimu ya msanii mwenye matatizo mengi Stevo Simple Boy.

Nyota Ndogo aliweka wazi haya kupitia ukurasa wake wa Facebook ambapo alieleza nia yake ya kutaka kumsaidia msanii huyo ambaye si mara ya kwanza kusaidiwa lakini baadae anajikuta katumbukia tena kwenye matatizo yale yale.

Akitoa wazo lake jinsi ya kumaliza kabisa matatizo yanayomkumba Stevo Simple Boy, Nyota Ndogo alisema kwamba kikwazo kikubwa ni kwamba hana elimu ya kusoma wala kuandika.

Mkali huyo wa ‘Watu na Viatu’ alisema njia pekee ya kuhakikisha Stevo ameondokea shida zake kwanza ni kumpa msaada wa kielemu ili ajue kusoma na kuandika, kwani hiyo ndio njia pekee ya kuweza kujisimamia kwa kila kitu.

Mimi nikipewa [Stevo] Simple Boy kwanza nampeleka shule angalau apate kaelimu kama kangu. Angalau ajue kusoma kidogo nakuandika. Hii hata sitachangisha maana nitamsomesha kulingana na uwezo wangu mdogo but naamini itamsaidia,” Nyota Ndogo alisema.

Pia msanii huyo alitoa sababu zake kuu kwa nini analenga kwa kumfadhili kimasomo na si kumsaidia kutoboa kimuziki.

Kwa maneno yake, Nyota Ndogo alisema;

“Nimesoma comment nyingi watu wanasema hajui kusoma wala kuandika. Ina maana account zake bila yeye kujua kusoma nakuandika hatawai kujua kuziendesha na ni muhimu ajue. Msichange arudishie account sababu bado hajui kutumia. Mimi mwenyewe sina elimu hivyo but najua kusoma kidogo nakuandika na inanisukumia siku mbele.”

Awali, Nyota Ndogo baada ya kufikiwa na habari kwamba msanii huyo ameripotiwa kurudi katika maisha yake ya zamani katika mtaa duni wa Kibera, aliibua kumbukumbu ya jinsi walivyokutana, akisema kwamba kwa taswira yake tu alimuona kama mtu mwenye shida.

Tulipokutana naye kwenye ile show Nairobi nilimuangalia nikamuhurumia sana sababu alikuwa ni kama mtu anayeendeshwa. Yaani anakuwa anacontroliwa. Fanya hivi fanya vile.”

“Huyu kijana asipopata usaidizi basi maisha yake yatapotea hivi hivi mkiona. Kwaufupi nahisi anateseka sana. Yaani nilitamani nimvute kando nimuambie kuhusu kazi anazopata nimshike mkono nimtafutie plot nimuongoze kujenga hata room mbili. Lakini hasimami peke yake. Yani amesimamiwa ili mtu asimsongelee kumchanua ama kumwambia chochote. Kilio cha msaada ndicho nilichoona kwenye macho yake,” Nyota Ndogo alikumbuka.