Msanii wa zamani wa Konde Gang, Anjella atangaza kuacha kuimba Bongo Fleva!

Anjella amekuwa akisuasua kimuziki tangu alipofanya uamuzi wa kugura lebo ya Harmonize mwishoni mwa mwaka 2022.

Muhtasari

• Akitetea hatua yake hiyo, Anjella anasema kwamba muziki wa Singeli ni muziki wa kiasili wa jamii za Uswahilini, na ndio maana ameamua kuukumbatia na kuachana na Bongo Fleva.

 

Anjella.
Anjella.
Image: Instagram

Msanii wa zamani wa Konde Music Worldwide inayomilikiwa na Harmonize, Anjella ametangaza kutundika daluga za muziki wa Bongo Fleva.

Kupitia insta story yake, Anjella amesema kwamba ameamua kugeukia muziki wa kiasili wa Singeli, akisema tayari ametayarisha albamu ya ngoma 20 za singeli.

Akitetea hatua yake hiyo, Anjella anasema kwamba muziki wa Singeli ni muziki wa kiasili wa jamii za Uswahilini, na ndio maana ameamua kuukumbatia na kuachana na Bongo Fleva.

“Nimeamua rasmi kuingia kwenye muziki wa Singeli. Nina albamu tayari yenye ngoma 20 na zote ni Singeli. Singeli ni muziki wetu wa asili,” Anjella aliandika.

anjella
anjella

Kando na Bongo Fleva, kwa nchini Tanzania muziki wa Singeli ni moja ya mdundo pendwa Zaidi ambao siku za nyuma ulikuwa unahusishwa na nyimbo za kitamaduni zilizoimbwa na wazee.

Katika miaka ya hivi karibuni, vijana wameonekana kujitosa katika utunzi wa muziki wa Singeli wakiwemo Dula Makabila, Dvoice na sasa Anjella.

Anjella amekuwa akisuasua kimuziki tangu alipofanya uamuzi wa kugura lebo ya Harmonize mwishoni mwa mwaka 2022.

Tangu kipindi hicho, hajakuwa akiachia miziki kwa kufululiza, na ukimya wake umehusishwa na kutokuwa imara katika kupata fursa nzuri ya kuketi chini na kutunga mashairi.

Licha ya kusema kwamba hakuondoka Konde Gang kwa shari, miezi michache iliyopita alimlipua Harmonize akidai kwamba msanii huyo ambaye alikuwa bosi wake huenda alikuwa moja ya vikwazo vikubwa katika kudidimiza nuru ya nyota yake wakati akiwa chini ya lebo yake.

Harmonize alikuwa amesema kwamba aliwapa Baraka wote walioondoka kwenye lebo yake lakini Anjella akamkaripia akitaka kujua ni Baraka gani wakati mwenyewe alikuwa anawakazia wasitoke.