Tamasha la Nyashinski la Marekani laghairiwa wiki mbili kabla ya kufika

Nyanshinski amelazimika kughairi ziara yake ya Marekani baada ya Visa yake kucheleweshwa.

Muhtasari

•Nyashinski ameghairi ziara yake ya muziki nchini Marekani iliyopangwa kufanyika Jumamosi, 1 Juni 2024.

•Nyashinski alikusudiwa kuwatumbuiza watu kwenye sherehe za Madaraka,nchini Marekani.

Nyashinski. Picha;Instagram
Nyashinski. Picha;Instagram

Msanii mahiri wa Kenya Nyamari Ongegu almaarufu Nyashinski ameghairi ziara yake ya muziki nchini Marekani iliyopangwa kufanyika Jumamosi, 1 Juni 2024.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo mwenye kipaji kikubwa amesema hatatumbuiza kwenye tamasha la USA Madaraka Festival 2024 kutokana na mambo yaliyo nje ya uwezo wa timu yake.

"Tunasikitika kutangaza kwamba kwa sababu ya mambo yaliyo nje ya uwezo wetu, hatutaweza kutumbuiza katika Tamasha la Madaraka la USA 2024", aliandika.

Akielezea masikitiko yake, aliendelea kusema kuwa licha ya juhudi kubwa za waandaaji wa tukio hilo, hawakuweza kupata visa kwa timu yake kuingia Marekani.

"Licha ya juhudi za waandaaji, hawakuweza kupata visa vya timu zetu kuingia Marekani. Tulikuwa tukitazamia sana ziara hiyo tunaomba radhi kwa usumbufu wote ambao umesababisha,” aliseam huku akiomba radhi

Siku zilizopita, Balozi wa Marekani nchini Kenya, Meg Whitman aliweka wazi kwa nini ubalozi wa Marekani huwanyima waombaji wengi visa. Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha runinga mnamo Mei 15, 2024, Whitman alisema  kwamba ubalozi umekuwa sahihi kukataa visa licha ya wengine kuwa na makosa.

Balozi huyo, akijibu swali, pia alieleza kwamba wanakataa visa katika kesi kama hizo ili kubaki macho na tahadhari kwa watu ambao wanaweza kuidhuru Amerika.

"Sisi huwanyima watu visa na je huwa tuna haki kila wakati? Hapana. Lakini je, tuko sahihi zaidi? Ndiyo. Fikiria kuhusu hilo kila mtu anataka kuja Amerika na baadhi ya watu wabaya wanataka kuja Amerika. Magaidi, wabadhirifu wa fedha, watu ambao wamekaa kupita kiasi. visa vyao hapo awali, watu ambao wameruhusu Green Card yao kuisha na kurejea," alisema.