6 wahukumiwa miaka 15 kwa mauaji ya aliyekuwa mbunge wa Juja George Thuo

Mjane wa Thuo alisema kuwa mumewe alilishwa sumu na kifo chake kilimpokonya mpenzi na baba ya watoto wake.

Muhtasari

• Mahakama iliwaepusha na adhabu ya juu zaidi, ikibainisha ripoti ya kuridhisha kutoka kwa ripoti ya majaribio.

Washukiwa sita wa mauaji ya mbunge wa zamani wa Juja

Watu sita waliopatikana na hatia katika mauaji ya aliyekuwa mbunge wa Juja George Thuo wamehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.

 Mahakama pia ilibainisha kuwa wana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Sita hao walipatikana na hatia ya kumuua mbunge huyo wa zamani mwaka wa 2013 katika klabu moja mjini Thika. 

"Mwishowe, ninamhukumu kila mshtakiwa, 1 hadi 6, kutumikia kifungo cha miaka 15," mahakama iliamua. 

Watu hao sita ni Andrew Karanja Wainaina, Paul Wainaina Boiyo, Christopher Lumbasio Andika,  Samuel Kuria Ngugi, Esther Ndinda Mulinge, na Ruth Vanessa Irungu. 

Mahakama iliwaepusha na adhabu ya juu zaidi, ikibainisha ripoti ya kuridhisha kutoka kwa ripoti ya majaribio na kusema hawakustahili hukumu iliyotolewa na sheria. 

"Jukumu la mahakama ni kusawazisha mizani ya haki... nitazingatia kipindi ambacho wamekaa rumande," mahakama ilibainisha. 

Mjane wa Thuo alipewa fursa ya kuzungumza mahakamani na kusema kuwa mumewe alilishwa sumu na kifo chake kilimpokonya mpenzi na baba ya watoto wake.