Michelle Ntalami amesherehekea mwaka mmoja bila kutumia pombe, miezi 2 baada ya kuokoka

Ntalami ambaye miezi miwili iliyopita alitangaza kuokoka, alifichua kwamba aliacha pombe hata kabla ya kupeana maisha yake kwa Mungu.

Muhtasari

• Ntalami ambaye miezi miwili iliyopita alitangaza kuokoka, alifichua kwamba aliacha pombe hata kabla ya kupeana maisha yake kwa Mungu.

MICHELLE NTALAMI
MICHELLE NTALAMI

Michelle Ntalami amesherehekea kumaliza mwaka mzima bila kutumia kileo chochote.

Kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, Ntalami alichapisha ujumbe mrefu akielezea jinsi amefanikiwa kwenye safari yake ya kuiasi pombe na  vilevi vyote.

Mrembo huyo alisimulia jinsi baadhi ya marafiki zake walimcheka mwaka jana alipoanza safari hiyo na kusherehekea siku za kwanza 30, wakisema kwamba hizo ni siku kidogo na angerudi katika unywaji wa pombe.

“Nasherehekea MWAKA MMOJA WA UTIMAMU!💧   Fikiri fam, mwaka mmoja kamili bila pombe! Na hiyo ni pamoja na shampeni na 'glasi isiyo na madhara ya mvinyo' iliyowahi kutetewa. Nakumbuka mwaka jana niliposhiriki kwa mara ya kwanza kwamba nilikuwa nikisherehekea hatua yangu muhimu ya siku 30, watu wengine walicheka na kusema siku 30 ni fupi sana na hivi karibuni nitarudi. hapo. Naam, tuko hapa, mwaka mzima!” alisema.

Ntalami ambaye miezi miwili iliyopita alitangaza kuokoka, alifichua kwamba aliacha pombe hata kabla ya kupeana maisha yake kwa Mungu.

“Kuacha pombe ni jambo ambalo nilifanya hata kabla ya kukutana na Mungu. Ingawa sikuwahi kuwa mraibu, haihitaji mtu kuwa mraibu kuacha tabia mbaya. Ikiwa kuna chochote, huo ndio wakati mzuri zaidi wa kuacha kwa kuwa una azimio zaidi la kuiacha kabla ya kufungwa.️ Kwa hivyo, takriban miezi 3 kabla ya hapo, niliacha kabisa kwenda kwenye vilabu na kuondoa/kutoa stash yangu. Nilianza kufanya mabadiliko chanya katika maisha yangu. Mabadiliko yalikuwa magumu lakini nilidhamiria kukata chochote na mtu yeyote ambaye hakuwa mzuri kwangu na kwangu,” Ntalami alieleza.

“Hii inakuambia kuwa haikuhitaji kufuata katika imani fulani kuacha tabia mbaya, hali au watu. Inawezekana kabisa kwa hiari yako mwenyewe. Huu ni moyo wangu wa dhati kwako wewe ambaye unafikiria kuachilia chochote. Mungu alitupa nia yetu wenyewe ya kufanya na kushikamana na maamuzi sahihi maishani. UNAWEZA KUFANYA,” aliongeza.

Miezi 2 iliyopita, Ntalami katika hali ya mshangao kwa wengi alitangaza kukutana na Mungu na kumpa maisha yake yote.