Muigizaji Idris Elba akabidhiwa ekari 80 za ardhi visiwani Zanzibar kujenga studio za filamu

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, studio hizo zinatarajiwa kuleta ushindani kwa zile zilizopo Bollywood, Nollywood na hata Hollywood, huku waziri huyo akidokeza kwamba huenda studio hiyo itaitwa Zollywood au Zawoo.

Muhtasari

• Shariff Ali Sharrif, waziri wa uwekezaji wa Zanzibar alithibitisha kwamba kulifanyika mazungumzo yaliyozaa matunda baina ya serikali na Idris Elba ambapo alikabidhiwa ardhi hiyo.

Idris Elba na rais Samia Suluhu Hassan.
Idris Elba na rais Samia Suluhu Hassan.

Muigizaji maarufu wa filamu za Hollywood, Idris Elba ameripotiwa kukabidhiwa ekari zaidi ya 80 za ardhi katika visiwa vya Zanzibar na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa studio za kisasa za filamu.

Kwa mujibu wa taarifa kwenye jarida la The Citizen, tangazo hilo liliwekwa wazi Alhamisi wiki jana wakati wa sherehe za awamu ya 27 za tamasha la kimataifa la filamu Zanzibar, ZIFF.

Shariff Ali Sharrif, waziri wa uwekezaji wa Zanzibar alithibitisha kwamba kulifanyika mazungumzo yaliyozaa matunda baina ya serikali na Idris Elba ambapo alikabidhiwa ardhi hiyo.

“Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dkt Hussein Mwinyi tayari imempa ekari 80 huko Fumba kuanzisha studio za kimataifa za filamu,” alinukuliwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, studio hizo zinatarajiwa kuleta ushindani kwa zile zilizopo Bollywood, Nollywood na hata Hollywood, huku waziri huyo akidokeza kwamba huenda studio hiyo itaitwa Zollywood au Zawoo.

Itakumbukwa mwezi Januari mwaka jana, Zuhura Yunus, aliyekuwa mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Samia Suluhu alitangaza kuwa kulikuwepo na mazungumzo baina ya rais na Elba kuhusu uwezekano wa jambo hilo.