Harmonize aeleza sababu ya kukataa kuimba Live wimbo ‘Nitaubeba’ aliomtungia Kajala (video)

“Ngoja kwanza, msalaba nimeshautupi sitaki masihara,’ Harmonize alisema kabla ya kurejea upande wa nyuma wa jukwaa.

Muhtasari

• “Ngoja kwanza, msalaba nimeshautupi sitaki masihara,’ Harmonize alisema kabla ya kurejea upande wa nyuma wa jukwaa.

HARMONIZE NA KAJALA
HARMONIZE NA KAJALA
Image: INSTAGRAM

Msanii wa lebo ya Konde music Worldwide, Harmonize aliwashangaza wengi wakati alipokataa kuwaimbia mashabiki wake mbashara kwenye jukwaa moja ya nyimbo alizotunga wakati penzi lake na Kajala lilikuwa ndio habari ya mjini.

Katika klipu ambayo inaenea kwenye mitandao ya kijamii, Harmonize alikuwa amejawa na bashasha tele jukwaani huku akitumbuiza kifua wazi kutokana na joto.

Kisha, mcheza santuri akaweka wimbo wake wa ‘Nitaubeba’ aliotunga mahsusi kwa ajili ya aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja.

“…nipo bize jamani na boo jamani nimeshasema, nipo bize na baby na msalaba wangu nitaubeba, na nitafika nao kiume. Nitaubeba iwe kwenye shinda na raha, ama kwenye shida na njaa na nitafika nao kiume,” kiitikio cha wimbo huo kiliimba.

Harmonize alirudi kwenye kipaza sauti akiwatazama mashabiki waliokuwa wameanza kuchangamkia wimbo huo na kusema kwamba hataki tena kuendelea kubeba msalama kwani ulishakuwa mzito na akalazimika kuutupa.

“Ngoja kwanza, msalaba nimeshautupi sitaki masihara,’ Harmonize alisema kabla ya kurejea upande wa nyuma wa jukwaa.

Harmonize waliachana na Kajala mwishoni mwa mwaka 2022, miezi 6 tu baada ya kurudiana kwa tafrija na mbwembwe tele zilizoshamili katika ukumbi wa Milimani City mwezi Juni mwaka huo.

Kabla ya Kajala kukubali kumrudia Harmonize, msanii huyo alikuwa amefanya msururu wa matukio ya kipekee kama vile kumnunulia gari jipya aina ya Range Rover na kutundika picha yake kwenye bango kubwa barabarani akimbembeleza kumrudia.

Kajala alikuwa amemuacha Harmonize mwaka 2021 katika kile kilichodaiwa kwamba ni alipopata uvumi kuwa msanii huyo ambaye alikuwa mpenzi wake alikuwa anamvizia binti yake, Paula.