Wajackoyah afurahi baada ya ndume aliyepewa jina lake kushinda vita vya ndume Kakamega

Wakili huyo msomi alichapisha video hiyo kupitia ukurasa wake wa Facebook, fahari wawili wakimenyana kwenye kinyang’anyiro hicho ambacho ni maarufu kwa jamii ya Magharibi mwa Kenya.

Muhtasari

• Makumi ya watu walikuwa wamezingira ndume hao wakimenyana huku kila mmoja akishabikia ndume anayempendelea.

• Hata hivyo, kama ilivyo katika mpambano wowote, sharti kuwepo na mshindi na mshinde, ndume mweusi aliibuka mshindi na kumpa Wajackoyah furaha isiyo na kifani.

WAJACKOYAH AFURAHI NDUME KUSHINDA
WAJACKOYAH AFURAHI NDUME KUSHINDA
Image: HISANI

Aliyekuwa mgombea wa urais, George Wajackoyah ameonesha furaha yake baada ya ndume aliyepewa jina lake kushinda pambano la fahali katika kaunti ya Kakamega.

Wakili huyo msomi alichapisha video hiyo kupitia ukurasa wake wa Facebook, fahari wawili wakimenyana kwenye kinyang’anyiro hicho ambacho ni maarufu kwa jamii ya Magharibi mwa Kenya.

Ndume wa rangi nyeusi ndiye aliyeitwa ‘Wajackoyah’ na alikuwa akipambana na ndume wa rangi ya kahawia aliyepewa jina ‘Mandela’.

Makumi ya watu walikuwa wamezingira ndume hao wakimenyana huku kila mmoja akishabikia ndume anayempendelea.

Hata hivyo, kama ilivyo katika mpambano wowote, sharti kuwepo na mshindi na mshinde, ndume mweusi aliibuka mshindi na kumpa Wajackoyah furaha isiyo na kifani.

“Hii ya ajabu. Fahali mpiganaji aliyeitwa kwa jina langu ashinda shindano la kumenyana kwa ng'ombe kati ya Kabras na Isukha huko Shinyalu kaunti ya Kakamega,” Wajackoyah aliandika kwenye video hiyo.

Baadae, Wajackoyah alifichua kwamba yuko nchini Jamaika kutangamana na baadhi ya mashabiki wake.

Alichapisha picha akiwa na mkali mtunzi wa muziki wa Reggae,m Richie Spice pamoja na meneja wake na kuelezea safari yake katika taifa hilo la Caribbean.

“Nikiwa na Richie Spice na meneja wake huko Kingston Jamaica. Walinikaribisha katika Hoteli ya kifahari ya Spanish. Nilifika Jamaika kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Montego Bay na kuendelea hadi Manchester kwa njia ya barabara. Kisha pa nilienda nyumbani kwa Bob Marley ya Nine Mile,” alifichua.

Wajackoyah ni mmoja wa wanasiasa wachache ambao wamekuwa wakipigia debe kuhalalishwa kwa bangi nchini na lilikuwa moja la azimio katika manifesto yake akiwania urais mwaka 2022.