Michelle Ntalami aandikia barua ya ushauri kwa wanachama wa LGBTQ

Ujumbe huu ulijiri saa chache baada ya kuweka wazi kwamba tangu ampokee Mungu, aliacha kujitambua kama mmoja wa wanachama wa LGBTQ.

Muhtasari

• “Rafiki zangu, hiyo ni njia mbaya, mnajihusisha na nguvu za kiroho za gizani, ambazo kina chake ni kirefu kuliko mnavyoelewa. Jiondoeni hapo kama mnaweza,” Ntalami aliongeza.

MICHELLE NTALAMI
MICHELLE NTALAMI
Image: INSTAGRAM

Michelle Ntalami ameandika barua ya kuwashauri wanachama wa mapenzi ya jinsia moja, LGBTQ akisema kuwa huo ni mrengo wa gizani ambao utawapeleka motoni.

Ushauri huu unakuja miezi michache tu baada ya Ntalami kudai wazi kwamba amejiondoa katika mrengo huo baada ya kuokoka na kumpokea Yesu kama mwokozi wa maisha yake.

Katika ushauri wake, alisema kwamba japo anaelewa wanayoyapitia na kwamba kila mtu ana uhuru wa kuchagua njia anayoiona ni sahihi, lakini njia ya LGBTQ ni ya kuelekea gizani.

“Kwa jamii ya LGBTQ na yeyote anayefanya kwa siri au wazi, nataka kusisitiza kwamba siwasuti. Ninaelewa changamoto zenu, ninawaombea kwa upendo na huruma. Hata hivyo, chaguo zetu, tamaduni na hisia huwa havielezei ukweli, lakini neno la Mungu pekee ndilo linaweza,” Ntalami alianza.

“Rafiki zangu, hiyo ni njia mbaya, mnajihusisha na nguvu za kiroho za gizani, ambazo kina chake ni kirefu kuliko mnavyoelewa. Jiondoeni hapo kama mnaweza,” Ntalami aliongeza.

Ujumbe huu ulijiri saa chache baada ya kuweka wazi kwamba tangu ampokee Mungu, aliacha kujitambua kama mmoja wa wanachama wa LGBTQ.

“Ninasimama kama mshindi katika jina lenye nguvu la Yesu Kristo, ninaposhiriki ushuhuda huu katika utii kwa Mungu. Tangu nilipokutana na Kristo maishani mwangu, sijitambui tena kama androsexual. Na kwa muda mrefu sasa, mimi si sehemu ya jumuiya ya LGBTQ+.”

“Nilichukua muda kumtafuta Mungu juu ya ngome hii iliyoenea katika ulimwengu wetu wa leo. Mungu Mwenyewe alinifunulia ukweli kuhusu njia hii na jinsi inavyoenda kinyume na mpango Wake wa Kimungu kwa wanadamu. Sasa ninaelewa kwamba ni shambulio la kiroho kutoka kwa shetani kwa kuwahadaa watu kutoka kwa kusudi lao la kweli na utambulisho wao,” Ntalami aliongeza.