Bradley Mtall amepewa ofa ya kazi nchini Serbia – Simon Kabu afichua

“Genz Goliath .. kuna kazi kwako hapa. Acha nimuunganishe na meneja wake ili kuuliza zaidi kujua kama ni halali na wafanye uamuzi sahihi,” Kabu alisema.

Muhtasari

• “Genz Goliath .. kuna kazi kwako hapa. Acha nimuunganishe na meneja wake ili kuuliza zaidi kujua kama ni halali na wafanye uamuzi sahihi,” Kabu alisema.

BRADLEY MTALL
BRADLEY MTALL
Image: FACEBOOK

Bradley Marongo maarufu kama Gen Z Goliath amedokezewa kupata ofa ya kazi nchini Serbia.

Kwa mujibu wa afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya kusafirisha watalii, Bonfire Adventures, Simon Kabu, alipokea ujumbe wa faragha kutoka kwa mtu anayedai kuwa na kazi nchini Serbia kwa ajili ya Bradley.

Kabu alionyesha ujumbe huo alioandikiwa na mtu huyo anayelenga kumpa Bradley kazi ukisema;

“Hujambo, unaweza pengine kutupatia Bradley Mtall, jamaa mrefu zaidi nchini Kenya. Tuko na kazi ya bure kwake hapa nchini Serbia. Inavyokaa, atalipiwa hadi nauli ya ndege. Kama unaweza tafadhali fuatilia hili kama pia yeye atakubali.”

Kabu alitoa taarifa hizo kwa furaha tele na kusema kwamba anaurudisha mpira kwa Bradley na meneja wake wapige tathmini ya hakika na kuona kama atakubali ofa hiyo ya kazi ama anaridhika na maisha yake nchini Kenya.

“Genz Goliath .. kuna kazi kwako hapa. Acha nimuunganishe na meneja wake ili kuuliza zaidi kujua kama ni halali na wafanye uamuzi sahihi,” Kabu alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Bonfire Adventures kumpa Bradley Mtall safari ya ndege kwa mara ya kwanza kuelekea Diani alikojivinjari kwa ziara iliyolipiwa ya siku 3.

Kijana huyo alipata umaarufu wakati wa kilele cha maandamano ya vijana wa Gen Z ambao walikuwa wanashiriki msururu wa maandamano kupinga utawala wa rais Ruto.