Mungu nihurumie, natubu kwa kumruhusu shetani kunitumia vibaya – Justina Syokau alia

Syokau alichapisha ujumbe wenye hisia za huruma akiomba msamaha kutoka kwa Mungu katika kile alidai kwamba ni kumruhusu shetani kumtumia vibaya katika siku za hivi karibuni.

Muhtasari

• Syokau alisema kwamba shetani amekuwa akitumia vibaya kinywa chake kutamka maneno ambayo si ya kupendeza machoni pake.

JUSTINA SYOKAU
JUSTINA SYOKAU
Image: HISANI

Msanii wa injili mwenye utata mwingi, Justina Syokau amerudi katika mitandao ya kijamii safari hii si kwa vitimbi vyake bali ni kwa mtindo wa kunyenyekea kwa Mungu.

Syokau alichapisha ujumbe wenye hisia za huruma akiomba msamaha kutoka kwa Mungu katika kile alidai kwamba ni kumruhusu shetani kumtumia vibaya katika siku za hivi karibuni.

Syokau alisema kwamba shetani amekuwa akitumia vibaya kinywa chake kutamka maneno ambayo si ya kupendeza machoni pake.

“Mungu nihurumie 😭😭 natubu kwa kumruhusu shetani anitumie 😭 kwa kutumia kinywa changu kunena mambo ambayo si sawa na mapenzi yako Mungu. Yesu nisaidie kuanzia leo nikuheshimu kwa kinywa changu,” Syokau alisema.

Msanii huyo pia aliomba Mungu kuwapa neema wale ambao amewakosea kumsamehe, akikiri kwamba amewakosea wengi tayari.

“Mungu nimewakosea wengi Mungu awasaidie wanisamehe, Mungu nipe neema ya kuwasamehe walio niumiza nahitaji kuanza tena Yesu na wewe. Nimekuaibisha Mungu, kuanzia leo nipe neema ili niishi maisha ya muumini nimeumizwa Mungu nahitaji moyo wa msamaha. Mungu nihurumie,” aliongeza.

Chapisho hilo liliwavutia wafuasi wake na umma mpana, ambao wengi wao wanafahamu historia ya Syokau ya kutoa kauli za ujasiri, mara nyingi zenye utata.

Syokau anayejulikana kwa wimbo wake wa injili wa ‘Twendi Twendi’, amesifiwa na kukosolewa kwa mtindo wake wa kuzungumza, ambao wakati mwingine umehusisha mijadala ya wazi ambayo inatia ukungu mistari ya maudhui ya jadi ya injili.