Mulamwah azungumzia kurejea uuguzi, afichua anachofanya ili kutosahau ujuzi wake

Alidokeza kwamba ataendeleza uuguzi katika siku za usoni baada ya kumaliza kazi yake ya sanaa.

Muhtasari

•Mulamwah aliweka wazi kuwa bado huwa anasoma sana ili kuhakikisha kuwa anafahamu mienendo katika fani ya uuguzi.

•“Nikishamaliza mambo haya ya mtandaoni baaas, mimi huyo bedside. Siwezi kusoma ivoo yote iende ivo,” alisema.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji wa Kenya David Oyando almaarufu Kendrick Mulamwah amefichua kuwa hafanyi kazi ya uuguzi kwa sasa.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mchekeshaji huyo ambaye alisomea kozi ya uuguzi katika chuo kikuu hata hivyo aliweka wazi kuwa bado huwa anasoma sana ili kuhakikisha kuwa anafahamu mienendo katika fani ya uuguzi.

Mulamwah alikuwa akijibu swali kuhusu ikiwa bado anafanya kazi ya uuguzi pamoja na kazi yake ya sanaa.

"Sio kwa sasa, siwezi kusimamia. Lakini nilisoma kila siku ili kusasishwa na mabadiliko ya sasa katika usimamizi wa huduma za afya na teknolojia,” Mulamwah alisema siku ya Jumatatu.

Mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 30 aliendelea kudokeza kwamba ataendeleza kazi yake ya uuguzi katika siku za usoni baada ya kumaliza kazi yake ya sanaa.

Wakati akimjibu mwanamtandao aliyemshauri kuhamia Marekani na kufanya kazi huko kama nesi, alisema kwamba hakusomea kazi hiyo ili kuiacha ipotee.

“Nikishamaliza mambo haya ya mtandaoni baaas, mimi huyo bedside. Siwezi kusoma ivoo yote iende ivo,” alisema.

Mchekeshaji huyo hivi majuzi amekuwa akivuma baada ya kudokeza kuwa yeye na ‘besti’ wake Ruth K, anayedaiwa kuwa mpenzi wake wanatarajia mtoto wao wa kwanza pamoja.

Wiki iliyopita, wawili hao walitangaza kwamba Ruth alikuwa akipata dalili ambazo kwa kawaida huhusishwa na ujauzito, na kuwaacha wanamitandao kukisia kuwa ni mjamzito.

“Bestie anatapika tapika ma asubuhi asubui ivi. Shida inaweza kua nini?" Mulamwah aliandika kwenye Instagram wiki jana.

Ingawa hawakuthibitisha ikiwa kweli walikuwa wakizungumza kuhusu ujauzito, wengi waliamini kwamba wawili hao walikuwa wakidokeza kutarajia mtoto pamoja.

Alipoulizwa kama Ruth bado anatapika, mcheshi huyo alibainisha kuwa kwa sasa mwili wake unazidi kuwa mkubwa na mkubwa.

“Kutapika imepungua. Kamwili ndio kananona tu sasa. I guess anakula poa,” Mulamwah alisema.

Mapema mwezi jana, Mulamwah alisema hana uhakika kama 'bestie' wake Ruth K ni mjamzito kama ambavyo Wakenya wamekuwa wakikisia.

Katika mahojiano na wanahabari, mchekeshaji huyo alifichua bado hakuwa amepata dokezo lolote kwamba Ruth anatarajia mtoto wake wa kwanza.

“Mimi sijui, mimi sijui, mimi siwezi kutarajia mtoto, ningekuwa nimesikia akigonga kwa tumbo. Lakini nitamuuliza,” Mulamwah alisema.

Pia alishikilia kuwa mrembo huyo ambaye amekuwa akiigiza naye ni rafiki yake tu na hakuna uhusiano wa kimapenzi kati yao.