Terence Creative afunguka jinsi nyanyake alivyomuokoa asikatwe miguu na madaktari

Mchekeshaji huyo alifichua kuwa madaktari walitaka kumkata miguu kwa sababu ilikuwa dhaifu sana.

Muhtasari

•Mchekeshaji Terence Creative amefichua kuwa ilikuwa nusura apoteze miguu yake akiwa mtoto kutokana na utapiamlo.

•Alisema nyanya yake alitatua hali yake kwa kumlisha matunda mengi yaliyosaidia kuimarisha miguu yake.

Image: INSTAGRAM// TERENCE CREATIVE

Mchekeshaji maarufu wa Kenya Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative amefichua kuwa ilikuwa nusura apoteze miguu yake akiwa mtoto kutokana na utapiamlo.

Wakati akizungumza katika kipindi cha Wicked Edition kwenye NTV, alifichua kuwa madaktari walitaka kumkata miguu kwa sababu ilikuwa dhaifu sana.

Mtumbuizaji huyo wa mbunifu alisema kuwa nyanya yake ndiye aliyezuia utaratibu huo kufanyika kwani kulikuwa na suluhisho mbadala kwa hilo.

“Nikiwa mdogo nilikuwa na miguu iliyogongana. Kwa kweli, ilikuwa nikatwe miguu juu ya utapiamlo, nyanya yangu akakataa. Nilikuwa natembea kidogo naanguka juu ya utapiamlo. Nimeteseka. Nitaandika kitabu,” Terence Creative alisema.

Alisema kuwa nyanya yake alitatua hali yake kwa kumlisha matunda mengi yaliyosaidia kuimarisha miguu yake.

“Miguu haikuwa na nguvu. Haikuwa na nguvu ya kusimama. Ilikuwa ikatwe, nyanya yangu alikataa akaambiwa anipee matunda. Na unajua alikuwa mama wa soko, sasa ni kunisukumia tunda moja baada ya linguine,” alisema.

Mchekeshaji huyo alibainisja kuwa matunda mengi ambayo nyanya yake alimpa yalisaidia kuipa miguu yake nguvu ya kushika mwili wake.

Huku akizungumzia maisha yake ya utotoni, mtumbuizaji huyo mashuhuri alifichua kwamba alilelewa katika mazingira duni sana.

“Mimi nimekulia Mlango Kubwa, eneo la Mathare. Majirani zetu wengi walikuwa Wakamba. Hapo tulikuwa tunakaa mimi, nyanya yangu, kaka watatu watatu na wajomba wangu wawili. Tulikaa watu kama wanane kwa chumba kimoja cha mraba. Mama yangu aliponizaa alinipeleka kwa mama yake. Yeye alikuwa anapitia hapo tu akiangalia kama niko. Mimi ndiye mzaliwa wa mwisho,” Terence alisimulia.

Terence alifichua kuwa alipokuwa akikulia Mathare hata aligeuka kuwa mtoto wa mtaani (chokora) kwa muda kwani hali nyumbani haikuwa rahisi. Wakati fulani maishani, yeye na kaka zake wakubwa pia walihusika katika uhalifu ambapo waliwasumbua wakazi kwa wizi.

Mtumbuizaji huyo pia alifichua kuwa wakati fulani maishani, alilelewa katika nyumba ya watoto huku kaka yake mkubwa pia alikua katika nyumba nyingine ya watoto. Kaka yake mzaliwa wa pili alibaki jijini Nairobi ambapo aliendeleza shughuli za uhalifu.