Terence Creative asimulia jinsi wizi nusura umpeleke yeye na kaka zake wakubwa kaburini

Terence alifichua kuwa yeye na kaka zake wawili wakubwa walikuwa wezi wakati fulani maishani mwao.

Muhtasari

•Terence alisimulia jinsi ndugu zake wakubwa walivyonusurika kifo baada ya kushambuliwa na watu kutokana na vitendo vyao vya uhalifu.

•Alifichua kuwa kaka zake wawili wakubwa walihusika katika wizi wa kiwango cha juu ilhali yeye mwenyewe alifanya wizi mdogo tu.

Image: INSTAGRAM// TERENCE CREATIVE

Mtumbuizaji maarufu wa Kenya Lawrence Macharia almaarufu Terence Creative amefunguka kuhusu maisha ya uhalifu ya zamani ya familia yao.

Wakati akizungumza katika kipindi cha Wicked Edition kwenye runinga ya NTV, alifichua kuwa yeye na kaka zake wawili wakubwa walikuwa wezi wakati fulani maishani mwao.

Mchekeshaji huyo mashuhuri alisimulia jinsi ndugu zake wakubwa walivyonusurika kifo baada ya kushambuliwa na umati wa watu wenye ghadhabu kutokana na vitendo vyao vya uhalifu.

“Kaka yangu, mzaliwa wa kwanza alipigwa kitutu nikamhurumia. Nilikuwa natazama na siwezi kusema kitu. Alipigwa bati, hao wasee walichukua mawe, wakamshika kichwa na wakamgonga gonga na ile mawe. Walimtoboa toboa kichwa,” Terence Creative alisimulia.

Alidokeza kuwa alishuhudia adhabu zote ambazo alikuwa akipewa kaka yake mkubwa lakini hakuweza kunena neno lolote kwani angeweza kuhatarisha kuhusishwa naye, na kuchochea umati huo kumshambulia pia.

Hata hivyo aliomba usaidizi wa polisi ili kuokoa maisha ya ndugu huyo wake.

“Nilienda kutafuta karao, juu alikuwa anapigiwa karibu na Pangani. Nikiita makarao, siwaiti nikiwaambia ni ndugu yangu, nawaambia kuna mwizi anapigwa pale endeni watamuua, endeni mumuone,” alisema.

Mchekeshaji huyo alisema kuwa polisi waliweza kuokoa maisha ya kaka yake baada ya yeye kuwakimbilia na akabainisha kuwa bado yuko hai hadi sasa.

Terence Creative pia alizungumzia jinsi kaka yake wa pili kuzaliwa alivunjika nyonga alipokuwa akipigwa na kundi la watu baada ya kufanya uhalifu.

“Kaka wangu wa pili alipigwa na mob wakamvunja nyonga. Huwa anatembea huku akichechemea. Huo ndio ushuhuda wake kuwa wizi sio poa. Sasa hata hatumhurumii. Lakini alibadilika, ni jamaa mzuri sana sasa," alisema.

Mtumbuizaji huyo alifichua kuwa kaka zake wawili wakubwa walihusika katika wizi wa kiwango cha juu ilhali yeye mwenyewe alifanya wizi mdogo tu.

Hata hivyo, aliweka wazi kuwa kwa sasa wote wamebadili njia zao na hawajihusishi tena na vitendo vya uhalifu.

“Waliacha uhalifu, ni watu wako na mabibi zao huko na watoto. Mwizi anaweza kubadilika ama siku zake 40 zifike,” alisema.

Terence pia alifunguka kuhusu jinsi yeye na kaka zake wawili walivyokua mbali na mwingine, huku yeye na kaka yake mkubwa wakilelewa katika nyumba ya watoto tofauti naye kaka yake wa pili akibaiki jijini Nairobi ambapo alifanya uhalifu.