Nyakati nzuri huku Waihiga Mwaura, Joyce Otieno wakisherehekea miaka 8 ya ndoa kwa njia ya kupendeza

Waihiga Mwaura na mkewe Joyce Omondi walisherehekea kumbukumbu ya miaka minane ya ndoa Jumatatu, Desemba 18.

Muhtasari

•Wapenzi hao walichagua kuwa na jioni ya kupendeza ya vyakula maalum vya kigeni, vinywaji na muziki mzuriwa kusisimua roho.

•Wanandoa hao mashuhuri walionekana wakiwa na nyuso za shangwe na tabasamu zuri nyusoni mwao .

 

Jotye Omondi na Mumewe Waihiga Mwaura
Image: INSTAGRAM// WAIHIGA MWAURA

Mwanahabari maarufu wa Kenya anayefanya kazi na BBC, Waihiga Mwaura na mkewe Joyce Omondi walisherehekea kumbukumbu ya miaka minane ya ndoa mnamo  Jumatatu, Desemba 18 kwa njia nzuri na ya kipekee.

Ili kuadhimisha siku yao maalum, wapenzi hao ambao kwa sasa wanafurahia likizo nchini Uzbekistan walichagua kuwa na jioni ya kupendeza ya vyakula maalum vya kigeni, vinywaji na muziki mzuriwa kusisimua roho.

Katika video walizoshiriki wawili hao kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii, walionekana kwenye mkahawa mmoja wakifahari ambapo walihudumiwa kwa vyakula mbalimbali vya kigeni huku bendi ya wapiga ala za muziki wakiwaburudisha.

"Chakula cha jioni cha leo kilikuwa cha kipekee... hii ilikuwa nzuri," Bi Omondi alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Wanandoa hao ambao walifunga pingu za maisha mnamo Desemba 18, 2015 walionekana wakiwa na nyuso za shangwe na tabasamu zuri nyusoni mwao walipokuwa wakifurahia siku yao ya kumbukumbu ya ndoa yao.

“Heri ya kumbukumbu mpenzi wangu!! #theonehekeptforme @waihigamwaura,” Bi Omondi aliandika kwenye video ya mwanamke akiwachezea kinubi.

Katika video zingine, wawili hao pia walionekana wakitembelea maeneo mengine mazuri na ya kufurahisha nchini Uzbekistan.

Wanandoa hao mashuhuri ambao nyuso zao ni maarufu sana miongoni mwa watazamaji wa Kenya kwa miaka mingi wamewashangaza wengi kwa muungano wao mzuri na jinsi ambavyo wamekuwa wakisherehekea kila mara.

Mwaka jana, Bi Omondi ambaye ni msanii wa nyimbo za injili alifichua kwa nini huwa hafichui mengi kuhusu ndoa yake kwenye mitandao ya kijamii, akisema ni kwa sababu ni jambo ambalo anathamini na anapendelea kulindwa dhidi ya macho ya umma.

"Sio siri kwamba nimeolewa lakini mimi huweka mambo ya faragha kwa sababu nilifunga ndoa na Waihiga pekee," alisema.

Aliongeza, “Kwangu mimi, ndoa yangu kwake ni ya kipekee sana, ni agano nililo nalo yeye na Mungu na nataka kulitunza na sikuweka nadhiri zangu kwa kila mtu, ni jambo ambalo nitalilinda na kulitunza. kuthamini namna hiyo."