Ombi maalum la marehemu Jahmby Koikai kwa rais Ruto kabla ya kifo chake

Kabla ya kuaga dunia Jumatatu usiku, marehemu Jahmby alikuwa ametoa ombi maalum kwa Rais William Ruto.

Muhtasari

•Jahmby alipoteza maisha katika Hospitali ya Nairobi siku ya Jumatatu usiku baada ya kuugua ugonjwa wa Endometriosis kwa muda mrefu.

•Jahmby amekuwa akipambana na ugonjwa wa Endometriosis kwa miaka mingi na kabla ya kifo chake aliwahi kulazwa hospitalini mara kadhaa.

alikuwa ametuma ombi maalum kwa rais William Ruto kabla ya kifo chake. Alifariki mnamo Juni 3, 2024.
Marehemu Jahmby Koikai alikuwa ametuma ombi maalum kwa rais William Ruto kabla ya kifo chake. Alifariki mnamo Juni 3, 2024.
Image: HISANI

Wakenya kutoka matabaka mbalimbali wameendelea kuomboleza kifo cha mtumbuizaji maarufu wa nyimbo za reggea Mary Njambi Koikai almaarufu Fyah Mummah Jahmby.

Jahmby alipoteza maisha katika Hospitali ya Nairobi siku ya Jumatatu usiku baada ya kuugua ugonjwa wa Endometriosis kwa muda mrefu. Alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi wakati alipofariki.

Kifo cha mtangazaji huyo maarufu wa nyimbo za reggae kinajiri siku chache baada ya kutuma pendekezo la afya kwa Rais William Ruto, wakati kiongozi huyo wa taifa alipokuwa katika ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Marekani.

Akitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii, Jahmby alimtaka Ruto pia kuzingatia matibabu ya ugonjwa wa endometriosis, akibainisha kuwa uwekezaji katika huduma za afya ni mojawapo ya maeneo muhimu ya ziara yake.

Jahmby, ambaye amepambana na ugonjwa wa endometriosis kwa muda mrefu, alieleza kwamba ni shauku kwa wasichana na wanawake wadogo wanaopambana na ugonjwa huo mbaya kupata matibabu yanayofaa katika hospitali ya kifahari iliyo Atlanta, Georgia.

“Huu ni wito wa dhati wa usaidizi kwa viongozi wachache wa Kenya, lakini niruhusu kwanza nizungumzie hili kwa Rais William Ruto anapofanya ziara yake nchini Marekani. Mheshimiwa Rais, moja ya mada muhimu katika ziara yako ni uwekezaji katika huduma za afya,” alisema.

"Atlanta, Georgia, ni jiji la ndoto kwa kila msichana mdogo na mwanamke ambaye amewahi kupambana na ugonjwa huu mbaya unaoitwa Endometriosis.

Kuna kituo ambacho kimejitolea kurejesha maisha ya wasichana na wanawake ambao wamelemazwa na ugonjwa huu. The @centerforendocare,” alieleza.

Jahmby alitaja maeneo ambayo angependa Rais Ruto atembelee ili kupata ufahamu kuhusu ugonjwa huo na jinsi wanavyoweza kuwasaidia wanawake wengi nchini Kenya.

"Unapoanza ziara yako Marekani, ningependa utembelee maeneo ambayo yangesaidia mamilioni ya wanawake wa Kenya kupambana na ugonjwa huu kimyakimya, kama vile Kituo cha Huduma ya Endometriosis na Kituo cha Wanawake katika Hospitali ya Northside," alifafanua.

Marehemu Jahmby amekuwa akipambana na ugonjwa wa Endometriosis kwa miaka mingi na kabla ya kifo chake aliwahi kulazwa hospitalini mara kadhaa.