Video ya kuhuzunisha ya msichana akivuka daraja hatari Kisii yaleta nuru katika kijiji chao

Eric Omondi alitangaza kuwa atafanya uchangishaji ili kupata pesa za ujenzi wa daraja hilo.

Muhtasari

•Eric alithibitisha alikutana na msichana aliye kwenye video hiyo, baba yake na wanakijiji na kuzungumza nao kuhusu hali ya daraja hilo.

• ”Jamii hadi sasa imejaribu Kuimarisha Daraja lakini haitoshi. Mbao Imeoza, Inatetemeka na HAIko SALAMA," Eric alisema.

akivuka daraja hatari
Mtoto akivuka daraja hatari
Image: HISANI

Mchekeshaji maarufu wa Kenya Eric Omondi amejitolea kusaidia jamii ya Kijiji cha Nyakumbati katika Kaunti ya Kisii kujenga daraja baada ya video ya msichana akivuka daraja jembamba sana iliyo juu ya mto uliofurika kusambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki jana.

Katika chapisho lake Jumanne alasiri, mchekeshaji huyo alithibitisha kwamba alikutana na msichana aliye kwenye video hiyo ambaye alifichua anaitwa Shirleen, babake Fred Ogata Mogire, na wanakijiji wengine ambao alizungumza nao kuhusu hali ya daraja hilo.

“Video ya kuhuzunisha ya msichana akivuka Daraja la mauti kwa ujasiri inatoka katika Kijiji cha Nyakumbati katika Kaunti ya Kisii. Msichana anaitwa Shirleen na Baba anaitwa Fred Ogata Mogire,” Eric Omondi alisema kwenye taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, ”Jamii hadi sasa imejaribu Kuimarisha Daraja lakini haitoshi. Mbao Imeoza, Inatetemeka na HAIko SALAMA. Ni suala la muda tu kabla ya kuanguka kwenye MSIBA. "

Aliendelea kutangaza kuwa atafanya uchangishaji ili kupata pesa za ujenzi wa daraja hilo.

“Anza Kutuma chochote unachoweza kwa Baba yake Shirleen kwa 0722115399 (JINA: FRED OGATA MOGIRE). TEAM SISI KWA SISI TUJENGE HII LEO, LETS GO!!!,” alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya video ya msichana huyo akivuka daraja hatari wakati akielekea shule kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia mseto kutoka kwa Wakenya.

Katika video hiyo ambayo ilisambaa wiki jana, msichana huyo mdogo alionekana akijaribu kuwa imara kwa kujishikilia kwenye miti iliyowekwa kando ya daraja hilo jembamba huku akivuka kwa umakini.

Msichana huyo alivalia sare ya shule ya buluu iliyokolea na begi mgongoni. Alionekana kuruka kutoka kwenye daraja na kupata utulivu anapomaliza kuvuka mto huo unaoonekana kuwa hatari chini yake.

Eric Omondi ni miongoni mwa watu waliotoa sauti zao kuhusu video hiyo huku akiwakashifu wanasiasa kwa kulegeza wajibu wao wa kujenga na kuboresha miundombinu kama vile daraja.

Mchekeshaji huyo alibainisha kuwa kwa kuvuka daraja hilo hatari, msichana huyo anakabiliwa na hatari ya kifo kwani mto ulio chini yake unaweza kumuua iwapo angeanguka.

“Hawa viongozi wanalalaje hata usiku??? Kwa hiyo msichana huyu mdogo anakabili kifo kila asubuhi. Akipiga hatua moja ndogo ya kukosea ndivyo hivyo😡, TUNAMPOTEZA!!! Huyu mtoto anaweza kupoteza maisha kwa sababu tu ya KIONGOZI MWENYE TAMAA, MTUKUFU na MUUAJI!!!” Eric Omondi alisema.

Wakati huo, alitangaza kwamba anamtafuta msichana huyo mdogo kwenye video hiyo na familia yake ili aweze kuwasaidia kuhamia mahali salama.

“Namtafuta huyu Msichana, inabidi tumuokoe. Tutamleta yeye na familia yake Nairobi. HATA KUVUKA TENA hili DARAJA LA MAUTI. Tafadhali TUMPATE. Ikiwa unatambua mahali hapa tafadhali toa maoni yako au tuma DM MAHALI.,” Eric alisema.