Willy Paul ajivunia maendeleo ya mwanawe wa kwanza, King Damian (+picha)

Willy Paul alisema mama ya mwanawe ni Mwarabu.

Muhtasari

•Huku akimsherehekea Damian siku ya Jumapili, mwimbaji huyo wa zamani wa injili alimtakia ulinzi wa Mungu siku zote.

• Ijumaa, Willy Paul alichapisha picha nzuri za mzazi mwenzake mzungu, Viktoriya Shcheglova na mtoto wao Sonya Wilsovna na kueleza jinsi anavyowapenda.

Mwanawe Willy Paul, King Damian

Siku chache tu baada ya kusherehekea familia yake ya Kirusi, mwimbaji wa nyimbo za mapenzi Wilson Radido almaarufu Willy Paul amemuonyesha upendo mtoto wake wa kwanza anayejulikana, King Damian.

Willy Paul alimtambulisha mwanawe huyo mara ya kwanza mwaka wa 2020 na amemuonyesha hadharani mara chache tu.

Huku akimsherehekea Damian siku ya Jumapili, mwimbaji huyo wa zamani wa injili alimtakia ulinzi wa Mungu siku zote. Willy Paul pia alionyesha kujivunia maendeleo ya mtoto huyo wake wa kwanza.

"Mwanangu Damian amekuwa mkubwa Waah! Damu moja, mama tofauti.. Mungu naomba ulinde familia yangu," alisema.

Bosi huyo wa Saldido aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri za Damian. Aliendelea kuwatakia mashabiki wake Jumapili njema.

Mwimbaji huyo alizungumza kuhusu mtoto huyo wake kwa mara ya kwanza katika mahojiano ya 2019 wakati Damian akiwa na mwaka mmoja.

Willy Paul alisema alikuwa akimficha mwanawe kwa kuwa mtu anayethamini usiri wake na ndiyo sababu hajamfungulia akaunti ya Instagram.

“Mimi btw niko na mtoto ako 12 months na mamake ni Mwarabu fulani tu anajielewa mbaya. Mtoto ni wa kiume anatwa King Damian jina lake la kwanza. Huyo ashakuwa staa tayari. Ni venye sinanga time ya umaarufu kidogo kwa sababu hujui huyu mtoto akikua kama hayo ndiyo maisha anapenda, kama anataka kuwa maarufu kama wewe ni msee anapenda akikua akuwe na maisha yake ya siri,” alisema.

Hata hivyo, hakuweka wazi hali ya uhusiano wake na mzazi mwenzake.

Siku ya Ijumaa asubuhi, mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili alichapisha picha nzuri za mzazi mwenzake mzungu, Viktoriya Shcheglova pamoja na mtoto wao Sonya Wilsovna na kueleza jinsi anavyowapenda.

Willy Paul alijivunia maendeleo ya binti huyo wake wa miaka minne na kufurahia jinsi alivyokua kuwa mkubwa.

"Mtazame binti yangu Sonya, amekuwa mkubwa! Muda haungojei mtu walahi. Nawapenda hawa binadamu wawili," alisema chini ya picha hizo.

Mwanamuziki huyo aliyezingirwa na utata mwingi kwenye taaluma yake ya takriban mwongo mmoja alihoji ni nini alichofanya ili kustahili familia nzuri kama hiyo. Pia aliahidi kuendelea kuachia muziki zaidi.