"Mama yangu ni mgonjwa sana" Willy Paul afunguka kwa uchungu

Mwimbaji huyo alighadhabika baada ya mwanahabari kutafuta kiki kutumia jina la mamake ambaye anaugua.

Muhtasari

•Mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi alisema amelifanyia kazi sana jina lake na kuweka wazi kwamba hatakubali lichafuliwe tena.

•Alifichua kuwa mamake kwa sasa anaugua, sababu iliyomfanya kuumia sana moyoni kuona jina lake likitumika kwa nia mbaya.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Willy Paul alishindwa kuzuia ghadhabu yake baada ya mwanahabari mmoja anayedai kuwa ni binamu yake kufanya ripoti akidai kuwa mama ya mwimbaji huyo anateseka katika umaskini huku mwanawe akiendelea kufurahia maisha mjini.

Huku akijibu kwenye ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul alimshutumu mwanahabari huyo kwa kutafuta kiki kwa kutumia jina lake.

Mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi alisema amelifanyia kazi sana jina lake na kuweka wazi kwamba hatakubali lichafuliwe tena.

"Nimefanya kazi sana kwa ajili ya jina hili. Nikiona jinsi watu hutumia jina langu kutafuta kiki inaniweka huzuni," alisema.

Willy Paul alidokeza kwamba katika nyakati zote ambazo watu mbalimbali wametafuta kiki kwa kutumia  jina lake, mwahabari huyo alimkasirisha zaidi kwa sababu ya kuburuta jina la mama yake ndani yake.

Alifichua kuwa mamake kwa sasa anaugua, sababu iliyomfanya kuumia sana moyoni kuona jina lake likitumika kwa nia mbaya.

"Hakuna kitu imeniuma kama hii. Yaani mama yangu ni mgonjwa sana alafu mtafuta kiki fulani anakuja kumtaja kwa uwongo? Basi angenitaja tu kwa sababu watu wamenizoea!!" aliandika Willy Paul siku ya Jumatano.

Msanii huyo alitaka yeyote anayemfahamu mwanahabari huyo kumwelekeza kwake huku akitaja ripoti hiyo kuwa ya kipuuzi.

Katika ripoti hiyo, mwanahabari huyo aliyedai kuwa mamake Willy Paul ni dadake mama yake  alimshtumu mwanamuziki huyo kwa kuishi maisha ya kifahari jijini Nairobi huku mzazi wake akiendelea kuishi maisha hohehahe katika nyumba ya ndogo ya udongo ambayo alionyesha kwenye video.