Chelsea wakubali meneja Maurizio Sarri ahamie Juventus

maurizio sarri
maurizio sarri
Chelsea wamekubali meneja wao Maurizio Sarri ahamie Juventus. Makubaliano yaliafikiwa jana kati ya maafisa wakuu na huenda yakatamatishwa hii leo.

Inaaminika kua ada ya takriban pauni milioni 5 ilikubaliwa. Sarri aliwasili kutoka Napoli Julai mwaka wa 2018 na kuwaongoza the Blues kwa nafasi ya tatu kwenye ligi ya Premier na kushinda ligi ya Uropa katika msimu mmoja alipokua meneja.

Kwingineko, mkurugenzi wa michezo wa Juventus Fabio Paratici amesafiri hadi katika afisi za Manchester United jijini Manchester kufanya mazungumzo ya ana kwa ana kuhusiana na uhamisho wa Paul Pogba.

Majadiliano yapo katika awamu za awali huku pia mchezaji wa Juventus Joao Cancelo akiaminika kuwa sehemu ya majadiliano hayo. Pogba aliondoka Juventus kuregea United mwaka 2016 kwa kitita cha pauni milioni 93.25.

Ajenti wa raia huyo wa Ufaransa, Mino Raiola sasa yuko huru kujadiliana na vilabu vya Italia baada ya marufuku iliyowekwa na ligi ya FA ya Italia kubatilishwa jana.

Tukisalia Uingereza, Liverpool hawana mpango wa kufufua mkataba na mchezaji wa Lyon Nabil Fekir, mwenye umri wa miaka 25, licha ya madai hayo yanayotolewa na Ufaransa.

Kwingineko, mshambuliaji wa Manchester United na Ubelgiji Romelu Lukaku, mwenye umri wa miaka 26, amekubali mkataba wa kibinafsi na Inter Milan katika mkataba unaoweza kumlipa nyota huyo pauni milioni 6.6 hadi mwaka 2024.