City Stadium kubadilishwa jina na kuitwa Joe Kadenge

City Stadium itabadilishwa jina na kuitwa Joe Kadenge Stadium kwa heshima ya gwiji huyo wa soka aliyefariki yapata wiki mbili zilizopita, kinara wa upinzani Raila Odinga alitangaza hapo jana.

Odinga anasema tayari ameshajadiliana na rais Uhuru Kenyatta na gavana wa kaunti ya Nairobi Mike Sonko kuhusu mipango ya kutekeleza hilo. Kadenge aliyejulikana sana kwa ustadi wake katika soka tangia miaka ya sitini atazikwa wikendi hii.

Kwingineko, kocha wa Harambee Stars Sebastian Migne anatarajiwa kuregea nchini hapo kesho baada ya mapumziko ya wki mbili kufuatia kushiriki katika kipute cha AFCON mwaka huu.

Migne anawasili siku moja kabla ya Stars kuripoti kambini kuanza matayarisho ya michuano ya kufuzu kwa CHAN mwaka wa 2020 ambapo watachuana na Tanzania wiki ijayo.

Mechi ya marudio itachezwa tarehe 4 mwezi ujao huku mshindi akipangiwa kupambana na Sudan katika raundi ya mwisho.

Tukisalia bara Afrika, aliyekua kiungo wa kati wa Uholanzi Clarence Seedorf amefutwa kazi kama kocha wa Cameroon baada ya timu hiyo kukosa kuhifadhi taji lao la AFCON.

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid alikua kwenye usukani kwa chini ya mwaka mmoja. Msaidizi wake Patrick Kluivert, pia amewachishwa kazi. Seedorf amesema alitaka kuendelea kama kocha na kwamba kikosi chake kimeonyesha dalili za kuimarika.

Huko Italia, nahodha wa Ajax Matthijs de Ligt aliwasili Turin jana jioni kukamilisha uhamisho wake wa pauni milioni 67.5 kwa mabingwa wa Serie A Juventus.