De Gea kusalia Old Trafford hadi 2023 baada ya kutia saini mkataba mpya

de Gea
de Gea
Kipa wa Manchester United David de Gea ametia saini mkataba mpya kusalia klabuni humo hadi mwaka 2023.

De Gea amechezea United mechi 367 tangu Sir Alex Ferguson kumleta klabuni humo kutoka Atletico Madrid kwa mkataba wa pauni milioni 18.9 Juni mwaka 2011.

De Gea, ambaye amechezea nchi ya Uhispania kwa mara 40, amesaidia United kushinda taji la ligi ya Pemier mwaka 2012-13, kombe la FA misimu mitatu baadae na pia kombe la ligi na ligi ya Uropa mwaka 2016-17.

Muhispania huyo ambaye amehusishwa na kuhamia Real Madrid hivi majuzi ,alikua katika mwaka wake wa mwisho wa mkataba.

Lionel Messi yuko katika kikosi cha Barcelona kitakachocheza mechi ya ufunguzi ya ligi ya mabingwa leo dhidi ya Borussia Dortmund baada ya kupona jeraha la mguu.

Nahodha huyo wa Barca alicheza mara ya mwisho Julai wakati wa Copa America akichezea Argentina na amekosa mechi nne za ufunguzi za Barca. Messi aliruhusiwa na madaktari kuregea baada ya mazoezi jana. Barca wameshinda mechi mbili tu kati ya nne za La Liga bila yeye.

Kwingineko, meneja wa Liverpool Jurgen Klopp anasema ushindi wao wa msimu uliopita wa ligi ya mabingwa hauwafanyi kuwa timu bora zaidi Uropa. Liverpool wanaanza utetezi wa taji hilo leo dhidi ya Napoli katika mechi yao ya ufunguzi ya kundi E na Klopp anasema kikosi chake hakiangalii ushindi uliopita.

Klopp anasema watajizatiti hata zaidi msimu huu huku wakitarajia ushindani mkali hasa kutoka kwa timu zinazotaka kuwalaza mabingwa hao.

Hayo yakijiri, mlinzi wa zamani wa  Manchester United Gary Neville anadai kuwa ajenti wa kiungo Paul Pogba, Mino Raiola ana tamaa na hafai kufanya biashara na klabu hio katika siku za usoni. Raiola ambaye hapo awali alipigwa marufuku nchini Italia kwa kuika kanuni za uuzaji wa wachezaji, anadai kuwa Pogba yuko tayari kuondoka ugani Old Trafford licha ya kuwa United hawataki kumuuza.

Neville anadai mvutano huo unaifanya hali ya Pogba kudorora uwanjani.