Noti za 1,000, Mkumbushe nyanya au mamako azibadilishe

Noti 1
Noti 1
Tafadhali mkumbushe mamako mzazi au nyanyako kubadilisha noti za 1,000 za zamani, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge ameonya.

“Mama zetu na nyanya wanapenda sana kuweka pesa kwa muda mrefu. Huenda wana noti za 1,000 za zamani pesa nyumbani mwao,” alisema siku ya Jumatano kwa Twitter.

“Tafadhali wachunguze na kuwakumbusha kuhusu siku ya mwisho ya matumizi ya noti za zamani za 1,000, Septemba 30 ili wabadlishane na noti mpya”.

Baada ya Septemba 30, noti za 1,000 za zamani hazitakuwa na thamani yoyote zitasalia karatasi tu. Wiki iliopita, Benki kuu ya Kenya ilisema kuna noti mpya za kutosha, na kutoa wito kwa wananchi kutumia fursa hii kubadilisha noti za 1,000 za zamani.

Takriban noti za zamani milioni 100, tayari zilikuwa zimerejeshwa kwa Benki Kuu ya Kenya kufikia mwisho wa mwezi Agosti kabla ya muda wa mwisho, Septemba 30.  Hii ni sawa na asilimia 50 ya noti za zamani zilizokuwa zikitumika, ina maanisha wananchi wana chini ya mwezi mmoja kurejesha noti milioni 117 za zamani kabla ya Oktoba Mosi.