Mke apatikana na maiti ya mumewe ndani ya nyumba ikiwa imeoza, adai anasubiri afufuke!

Majirani walisema kuwa mwanamke huyo na mumewe walikuwa washiriki wa dhehebu la kidini linalozuia matumizi ya vyakula, isipokuwa ndizi na matikiti maji.

Muhtasari

• Maafisa hao waliingia kwa nguvu ndani ya nyumba ya mwanamke huyo baada ya kuwanyima kibali cha kuingia, na kupata maiti ikiwa imelala kando ya kitanda chake sebuleni mwake.

Picha ya maktaba ya gari la Polisi katika eneo la uhalifu.
Image: MAKTABA

Mwanamke mmoja katika mji wa Kitengela kaunti ya Kajiado amekamatwa na polisi baada ya kupatikana na maiti ya mumewe ndani ya nyumba ikiwa imeoza.

Kwa mujibu wa ripoti ya Citizen, mama huyo wa miaka 58 alikuwa ameishi na maiti ya mumewe nyumbani kwa siku kadhaa, akidai kwamba alikuwa anamsubiri kufufuka ili maisha ya ndoa yaendelee.

Polisi walivamia nyumba hiyo baada ya majirani kuwafahamisha kuhusu harufu ya ajabu kutoka kwa boma la mwanamke huyo.

Maafisa hao waliingia kwa nguvu ndani ya nyumba ya mwanamke huyo baada ya kuwanyima kibali cha kuingia, na kupata maiti ikiwa imelala kando ya kitanda chake sebuleni mwake.

“Polisi waliingia ndani ya boma na kumkuta mwanamke huyo akiwa peke yake. Alionekana mgonjwa, amechoka na amedhoofika. Kwa kweli alikuwa akitetemeka sana,” kilisema chanzo kilichonukuliwa na Citizen.

Kulingana na majirani, mwanamke huyo alidai kuwa alikuwa ameuweka mwili huo ukisubiri ufufuo wake.

Majirani walisema kuwa mwanamke huyo na mumewe walikuwa washiriki wa dhehebu la kidini linalozuia matumizi ya vyakula, isipokuwa ndizi na matikiti maji.