OCS adaiwa kuficha nguo ya washukiwa korokoroni

Watu wawili walifikishwa kortini Jumanne wakiwa uchi. Watuhumiwa hao walielekeza lawama kwa OCS wa Kamukunji kwa kuwadhalilisha, na kuwalazimisha kuvua nguo zao na kuzichukua.

Peter Gatimo ambaye alifikishwa kizimbani akiwa amevaa tu kaptula yake ya ndani alielezea kuwa alikamatwa ijumaa na kuagizwa kuvua nguo zote na afisa ambaye alikuwa anasimamia kituo hicho lakini jina lake halikutajwa.

Gatimo alidai kuwa maafisa hao hawangeweza kumfikisha mahakamani siku ya jumatatu kama inavyotakiwa kisheria kwani walidai kuwa hawangeweza kupata nguo yake. Gatimo aliongeza kuwa alipewa nguo zingine avae ambazo hazikuwa zinamtoshea lakini alikataa kuzivaa.

Mtuhumiwa mwingine Jimmy Ndirangu alifikishwa mahakamani akiwa amevalia kaptula ya ndani pekee kwani alikataa kuvaa nguo chafu ambazo alikuwa amepewa na maafisa hao avae.

Wawili hao walifikishwa mbele ya hakimu Angelo Kithinji ambaye alimuagiza afisa wa upelelezi kuuliza OCS kuhusu tuhuma hizo mbili tofauti ya wizi wa nguo za wafungwa.

Gatimo anashtakiwa kwa wizi na vurugu mnamo septemba 12 katika kituo cha basi OTC, kando ya barabara ya racecourse jijini Nairobi.