Fuvu la kichwa cha Cohen lilipasuliwa na wauaji wake

Wauwaji wa aliyekuwa bwenyenye wa mchezo wa gofu Tob Cohen walivunja fuvu la kichwa chake, mguu wake wa kushoto na mkono wake alipokuwa anajaribu kupigana nao ili kujiokoa.

Picha za mwili wa Cohen siku ya Jumanne zilifichua mateso aliopitia afisa huyo mkuu wa zamani wa Phillips mikononi mwa wauaji wake.

Picha hizo kulingana na Jarida kuu nchini Uholanzi Algemeen Dagblad (AD), zilionyesha kuwa Cohen aliteswa kabla ya kuzidiwa nguvu na wauaji wake katika mauaji ya kikatili zaidi siku za hivi majuzi.

Imefichuliwa kwamba chembe chembe za DNA zilizochukuliwa kutoka ndani ya kucha za marehemu zitatoa muongozo muhimu kusaidia kutambua waliomuua wakati uchunguzi kamili utakapokamilika.

Mwili wa bwenyenye huyo mholanzi uliokuwa umeanza kuoza ulipatikana Ijumaa alasiri wiki iliyopita katika tanki la chini ya ardhini nyumbani kwake katika mtaa wa Kitusuru, majuma manane baada ya kutoweka.

Ulikuwa umefungwa mara kadhaa ndani ya mifuko ya plastiki. Cohen aliripotiwa kutoweka kutoka boma lake la Lower Kabete jijini Nairobi mnamo Julai 19 na 20.

“Mwili wake ulionyesha dalili za kuteswa, polisi walisema.

Cohen aliuawa katika njia ya kutisha. Mikono yake,miguu na shingo vilifungwa.

Wauaji walichukuwa muda wao, "DCI George Kinoti alisema baada ya mwili wa Cohen kupatikana Ijumaa iliopita.

Zoezi la kufanyia mwili huo upasuaji lililokuwa limesubiriwa kwa hamu sana lilifanyika siku ya Jumatano katika chumba cha kuhifandhia maiti cha Chiromo na kuhudhuriwa na mjane Sara Wairimu, dadake Cohen, Gabrielle Cohen, afisa wa uchunguzi na watu wangine wa familia hiyo.

Wairimu aliyeletwa chini ya ulinzi mkali na maafisa wa magereza, mapema alikuwa ametofautiana na Gabrielle kuhusu utaratibu wa kufanyia mwili huo uchunguzi.

Wawili hao walikabiliana vikali kuhusu ni muda upi Wairimu, ambaye ni mshukiwa mkuu katika mauaji ya Cohen, alistahili kuwa katika eneo hilo na nani angetambua mwili wa marehemu.

Makabiliano baina ya wawili hao karibu yasambaratishe shughuli ya upasuaji wa mwili siku ya Jumatano.

Katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Chiromo, utata kuhusu nani anafaa kupewa mwili kwa maziko pia uliibuka huku familia ya Cohen ikisisitiza kupewa mwili naye Wairimu akidai kuwa na haki ya kumzika mumuwe.

Gabrielle anataka kupewa mwili wa kakake ili amzike haraka iwezekanavyo kabla ya kurejea nyumbani kwao Uholanzi. Wairimu kupitia wakili wake Phillip Murgor naye alisema hataruhusu mtu yeyote kuuchukuwa mwili wa mumewe.