Wazazi, wanafunzi wa Precious Talent School wasimulia mkasa

precious talent
precious talent
Wazazi walipowapeleka watoto wao shule ya Precious Talent katika Dagoretti kusini Ijumatatu asubuhi, kila mmoja wao alitarajia kwamba wanao  wangerejea jioni na kujumuika nao kama desturi.

Kile hawakufahamu ni kwamba jicho la mauti lilikuwa limewakodolewa 8 kati yao katika majengo ya shule hiyo.

Shule hiyo ilikuwa ya ghorofa mbili na ilikuwa imejengwa kwa mbao na mabati juu ya jengo la zamani.

Naibu wa Rais Ruto asema kwamba serikali imewapa eneo hilo  la Dagoretti South Sh 10 milioni  za kujenga shule za msingi.

Takribani wanafunzi 64 walijeruhiwa  katika mkasa huo.  Wanafunzi 60 walitibiwa katika hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta  na kuruhusiwa kwenda nyumbani jana.

Baadhi ya wanafunzi waliarifu Radio Jambo kwamba waligundua jengo hilo lilikuwa limeinama  na mpindo, mvulana mmoja akamwarifu mwalimu ambaye alimweleza asiwe na hofu na akaambiwa arudi darsani.

Wazazi waliojawa na hofu walijumuika katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta huku wakisubiri taarifa kuhusu hali za wanao. Walisimulia kwamba shule hiyo imekuwa ikifinya vyema katika mitihani na gharama yake haikuwa ghali sana ijapokuwa ni shule ya kibinafsi.

Miongoni mwa wanafunzi ni Anthony ambaye alikuwa ameketi kimya darsani  Jumatatu asubuhi  akidurusu huku mwalimu wake akiwa mbele akitayarisha ratiba ya siku. "Niliwasili shuleni saa 6 asubuhi na mwalimu akatueleza tusome  kwa kuwa wanafunzi wote  hawakuwa wamewasili." alisema.

"Jiwe liligonga mguu wangu wa kushoto, nilihisi maumivu makali sana lakini nikabahatika kutorokea  nje na nikapatana na wanafunzi wengine waliojeruhiwa." Anthony alisema.

Walitoka nje wakipiga mayowe huku wakisubiri kuokolewa.

Chebet ambaye ni dadake alikuwa kazini alipoarifiwa kuhusu maporomoko ya jengo la shule hiyo. Alisema kwamba alishtuka sana baada ya kumkosa kaka yake mdogo katika hosipitali yote alioenda kumtafuta.

"Nilikuwa na wasiwasi sana nilipofika  hospitali ya Kenyatta, hatukuruhusiwa kungia wodi na kuona majeruhi ila tuliambiwa tukae katika mapokezini na kupewa majina ya wanafunzi waliokuwa hospitalini." alisema.

Aligundua baadaye kwamba kakake alikuwa shwari baada ya amu wake kufanikiwa kuingia kwenye wodi na kumwona alikolazwa. Ingawa alikuwa na tabasamu moyoni kwa kumwona akiwa hai, furaha yake iligubikwa na majonzi alipoambiwa kuhusu mauti ya mtoto wa darasa la 1 ambaye alikuwa jirani wake.

Mwana wa Elias OKoth alikuwa akidurusu baada ya kupelekwa shuleni na baba yake mwendo wa 6.45 asubuhi. Alipokuwa akirejea nyumbani, OKoth anasimulia kwamba alipatana na mwendeshaji boda boda ambaye alimwarifu kwamba shule  iliyokuwa karibu imeporomoka.  Huku akiwa na hofu asijue la kufanya, Okoth ambaye ni baba wa watoto wawili alikimbia shuleni kushuhudia kilichojiri.

Alipatwa na mshangao pale alimpompata mwanawe akiwa amefunikwa na kifusi. "Nilimpeleka mtoto wangu shuleni asubuhi na hata tukazungumza na mwalimu wake kabla ya kuerejea kwa shughuli zangu za kawaida. Nilipofika shuleni nilipata jengo lote limeporomoka. Baadhi ya wanafunzi walikuwa wamefunikwa na vifusi huku baadhi yao wakifanikiwa kutorokea usalama. " alisema . Alielezwa kwamba manawe alipelekwa kwenye dispensari ya Saint Sacred Church.

Afisa msimamizi wa hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Evanson Kamuri  alisema kwamba wanafunzi wengi hawakuwa wamejeruhiwa sana. " Ni wanafunzi wawili tu ambao waliumia sana, tumewafanyia CT scans na X-ray na uchunguzi zaidi na madaktari," alisema.