Kaunti ya Nakuru yatupa nje mswada wa Punguza mzigo

aukot
aukot
Bunge la kaunti ya Nakuru limekuwa la nane kukataa mswada wa Punguza mzigo unaofadhiliwa na chama cha Thirdway alliance kinacho ongozwa na Ekuru Aukot.

Mswada huo uliowasilishwa na mjumbe wa eneo la Naivasha Biashara Erick Gichuki ulitupwa nje baada ya aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge hilo Stanley Karanja kukataa kuunga mkono.

Karanja alisema kuwa idadi kubwa ya wajumbe walidokeza kuwa mswada huo ulikuwa unapendekeza kuwa maeneo bunge yapunguzwe, jambo ambalo kulingana na wao utaathiri wadi kadhaa.

Tayari  Siaya, Homabay, Nyamira, na Murang'a ni miongoni mwa kaunti ambazo zimeshajadili muswada huo na kukosa kuupitisha.

Kaunti ya Uasin Gishu pekee ndiyo imepitishwa mswada huo.

 Sheria iliyopendekezwa inakusudia kufanya mabadiliko, pamoja na kupunguza bajeti ya kila mwaka ya bunge kutoka shilingi bilioni 36.8 hadi shilingi bilioni tano.

Vile vile inapendekeza kupunguza idadi ya wabunge kutoka 416 hadi 147 na kuanzisha kipindi cha miaka saba ya Urais.

Angalau maeneo bunge 24 yanapaswa kupitisha mswada huo ili ufikishwe katika bunge la kitaifa na seneti kwa idhini.

Ikiwa wabunge wengi watauunga mkono, mswada huo utawasilishwa kwa Rais kwa idhini.