Rais Kenyatta afariji mama na mtoto waliofariki katika ajali ya feri ya Likoni

Rais Uhuru Kenyatta anatuma risala ya rambirambi na faraja kwa familia ya Bw. John Wambua ambaye alimpoteza mkewe Mariam Kighenda na bintiye Amanda Mutheu katika mkasa wa feri  uliofanyika katika kivukio cha  Likoni.

Risala ya rambirambi kutoka kwa Rais imetumwa baada ya kukamilika kwa shughuli za kutafuta na kutoa gari na miili ya waliofariki katika mkasa huo, shughuli ambayo ilitekelezwa na kundi la wataalamu kutoka idara zetu mbali mbali.

Rais amehuzunishwa na tukio hilo na anawahakikishia Wakenya wote kwamba hatua zinachukuliwa kuhakikisha kisa kama hicho  hakitatokea tena katika siku za usoni.

Mbali na ukarabati wa huduma za feri unaoendelea, Rais anasema Ujenzi uliopendekezwa wa Daraja la Likoni, ujenzi unaoendelea wa  barabara ya Dongo Kundu na pia kukamilishwa kwa barabara ya Samburu-Kinango-Kwale kutasaidia kupunguza msongamano katika kivukio hicho cha baharini kati ya Kisiwa cha Mombada na Kusini mwa Pwani.

Rais ambaye amekuwa akifuatilia kwa makini shughuli za kutafuta na kutoa gari na miili hiyo katika muda wa  siku 13 zilizopita, anapongeza kundi la wataalam waliohusika kwa bidii yao kuhakikisha kufaulu kwa shughuli hiyo  ambayo imechukua muda mrefu, ya kuchosha na ya hatari.

Kwa familia ya Bw.Wambua, Rais anaihakikishia kwamba serikali itaendelea kuwasaidia huku wanapoomboleza wapendwa wao.

-PSCU