Je Magufuli anataka kumgeuza Harmonize kuwa mwanasiasa? Pata uhondo

harmonize
harmonize

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa anatamani msanii, Rajab Abdul maarufu kama Harmonize au 'konde boy' kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Tandahimba mkoani Mtwara, limeripoti gazeti la Mwananchi nchini Tanzania.

Rais Magufuli amesema hayo katika mkutano wa hadhara, mara baada ya msanii huyo kutumbuiza katika mkutano huo huko mkoani Lindi.

Harmonize amekuwa akikaribishwa kutumbuiza katika mikutano mbalimbali ya hadhara inayofanywa na rais Magufuli mara baada ya kutoa wimbo wake wa Magufuli.

Wimbo huo wa Magufuli ulioimbwa kwa mdundo wa wimbo wake wa zamani ya Kwangaru, umemsifu Magufuli kwa kazi aliyoifanya katika taifa hilo.

"I wish ningemuona Magufuli nimpigie magoti na kumpongeza hadharani...mchapakazi hachoki...Fly over sasa tunazo, Airport imeshajengwa...acha nikupongeze kwa Air Tanzania..." wimbo wa Harmonise unaoitwa Magufuli.

Lakini swali ni je, mwanamuziki huyo ataonesha nia kwa uchaguzi ujao ambao maandalizi ya uchaguzi tayari yameanza?

Iwapo Harmonize atagombea wadhfa huo wa ubunge basi anaweza kuwa msanii wa kwanza maarufu kuchukua kiti cha ubunge kupitia chama tawala.

 Kwa Afrika mashariki , mwanamuziki kuwa kiongozi sio jambo geni. Tayari taifa hilo limekuwa na viongozi ambao ni wabunge ingawa wote wanatokea chama cha upinzani.
Msanii wa bongo fleva Joseph Haule maarufu kwa jina 'Profesa Jay' alipata ubunge wa jimbo la Mikumi mkoani Morogoro tangu mwaka 2015 mpaka sasa.

Profesa Jay alipata wadhfa huo baada ya kutoa wimbo wake uliotamba wa 'Ndio mzee' ambao ulikuwa unaeleza namna kiongozi anaweza kutoa ahadi bila kuzitimiza.

Msanii mwingine maarufu nchini humo ni Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr.Two au Sugu amekuwa mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama cha upinzani cha chadema nchini humo tangu mwaka 2010 mpaka sasa.

Mwaka 2018, Joseph Mbilinyi alishtakiwa kwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya rais Magufuli na kutumikia kifungo cha miezi mitano.

Je? Harmonize ataufuta mtindo huo?

BBC