Kwa nini serikali imelazimika kusimamisha shule kufunguliwa na kuahirishwa hadi wiki ijayo

Shule zilipangwa kufunguliwa tena leo Jumatatu, Aprili 29.

Muhtasari

•Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema wamepokea data kwamba baadhi ya shule zimeathiriwa vibaya na mafuriko yanayoendelea.

•Waziri Machogu alisema Wizara yake itashirikiana na mashirika na wadau husika kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mvua.

 

akizungumza alipoongoza utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Wakfu wa KCB mtaani Karen, Nairobi Januari 17, 2023.
Waziri wa elimu, Ezekiel Machogu akizungumza alipoongoza utoaji wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Wakfu wa KCB mtaani Karen, Nairobi Januari 17, 2023.
Image: LEAH MUKANGAI

Serikali kupitia wizara ya elimu imeahirisha kufunguliwa kwa shule hadi Jumatatu, Mei 6, 2024.

Katika taarifa yake ya Jumapili, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alisema wamepokea data kwamba baadhi ya shule zimeathiriwa vibaya na mafuriko yanayoendelea.

Alisema kuwapeleka wanafunzi na wafanyikazi katika shule zilizoathiriwa itakuwa kuweka maisha yao hatarini, kwa hivyo uamuzi wa kuahirisha kufunguliwa tena.

"Athari mbaya za mvua katika baadhi ya shule ni kubwa sana hivi kwamba haitakuwa jambo la busara kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wafanyikazi kabla ya hatua za kuzuia maji kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa kutosha wa jamii zote za shule zilizoathiriwa.

“Kutokana na tathmini hii, Wizara ya Elimu imeazimia kuahirisha kufunguliwa kwa shule zote za msingi na sekondari kwa wiki moja hadi Jumatatu, Mei 6, 2024,” Machogu alisema.

Shule zilipangwa kufunguliwa tena  leo Jumatatu, Aprili 29.

Waziri Machogu alisema Wizara yake itashirikiana na mashirika na wadau husika kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mvua.

Aliongeza kuwa pia watatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo yote yanayohusu sekta ya elimu.

Haya yanajiri muda mfupi baada ya Muungano wa Kitaifa wa Wazazi kupendekeza mabadiliko ya tarehe za kufunguliwa kwa shule katika maeneo yaliyoathiriwa siku ya Jumapili.

Haya yanakuja huku idara ya utabiri wa hali ya anga ikionya kuhusu mvua kubwa zaidi katika siku zijazo huku zaidi ya watu 90 wakiripotiwa kufariki na wengine wengi kujeruhiwa au kutoweka.

Kulingana na Katibu Mkuu wa muungano huo Eskimos Kobia, makumi ya shule kote nchini zimeathiriwa na mvua na mafuriko.

Kobia aliitaka serikali kukagua idadi ya shule zilizoathiriwa na mvua kwa lengo la kubadilisha tarehe za kufunguliwa kwa usalama wa wanafunzi na walimu.

"Tunafuatilia kwa makini mvua zinazoendelea kunyesha na tunashirikiana na serikali ili maisha ya wanafunzi yawe salama shule zinapofunguliwa kwa muhula wa pili," alisema.