Bodi ya utumishi wa umma ya Busia yajipata motoni kuhusu uajiri

MCA Gardy Jakaa alitaka maelezo kuhusu jinsi barua za uteuzi za watu fulani zilivyoondolewa na nafasi zao kuchukuliwa na wengine

Muhtasari

• Kamati iliibua hoja juu ya maofisa ambao wanadaiwa kuajiriwa bila kuteuliwa wala kuhojiwa kwa nafasi walizopewa. Tuhuma hizo hata hivyo zilikanushwa vikali na Onyura.


Vikao vya bunge la Kaunti ya Busia
Vikao vya bunge la Kaunti ya Busia
Image: HISANI

Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti ya Busia ilikuwa na wakati mgumu kueleza madai ya kasoro na upendeleo katika uajiri wa hivi majuzi wa wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa idara mbali mbali.

Akiwa mbele ya Kamati ya Leba, Haki za Binadamu na Ustawi wa Jamii, mwenyekiti wa Bodi ya Utumishi wa Umma Mhe. Michael Onyura alitakiwa kuangazia kilio cha umma kuhusu madai ya upendeleo na ufisadi katika bodi hiyo.

Kamati iliibua hoja juu ya maofisa ambao wanadaiwa kuajiriwa bila kuteuliwa wala kuhojiwa kwa nafasi walizopewa. Tuhuma hizo hata hivyo zilikanushwa vikali na Onyura.

“Naweza kuithibitishia kamati hii tukufu kwamba hakuna mtu aliyeajiriwa bila kufuata utaratibu,” alisema Onyura.

Mwenyekiti wa Bodi alitakiwa kueleza jinsi mtu asiye na uzoefu na ujuzi stahiki alivyopewa kuongoza idara moja muhimu.

Mwakilishi wadi Gardy Jakaa (Bukhayo Kaskazini) alitaka maelezo kuhusu jinsi barua za uteuzi za watu fulani zilivyoondolewa na nafasi zao kuchukuliwa na wengine ambao ilidaiwa hawakuwa wamefuzu kwa nyadhifa hizo wakati wa mahojiano.

"Ni wakati gani bodi iligundua barua hizo zilitolewa kinyume na utaratibu na bodi imechukua hatua gani dhidi ya mwanachama wake aliyetoa barua hizo," aliuliza Jakaa.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo MCA Patrick Omanyala alimuuliza mwenyekiti wa Bodi kwa nini orodha ya waliyofaulu iliondolewa mara moja kwenye tovuti baada ya ya hoja ya Jakaa kupitishwa na bunge. Bodi kwa upande wake ilisema orodha hiyo iliyoondolewa haikuwa imeidhinishwa kupakiwa kwenye tovuti ya kaunti.

MCA wa Bukhayo Magharibi Peter Tallam alitaka maelezo kuhusu jukumu la idara ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma katika mchakato wa kuajiri. Afisa Mkuu Patricia alisema jukumu la idara hiyo ni kuhakikisha watu walioteuliwa wamewekwa kwenye orodha ya malipo.

Kamati ya bunge la kaunti ilitazamiwa kuanza kuandaa ripoti ya matokeo yake na kuwasilisha Bungeni ndani ya siku 14. Uchunguzi huo ni hitimisho la hoja iliyotolewa na Gardy Jakaa akitafuta maelezo kuhusu mchakato mzima wa kuwaajiri wakurugenzi na manaibu wakurugenzi katika kaunti ya Busia.