Mama wa Taifa Margaret Kenyatta kuendelea kutetea usawa wa kijinsia

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta leo amekariri kujitolea kwake kuendeleza mipango ya kuboresha usawa wa kijinsia na kuwapa uwezo wanawake nchini.

Mama wa Taifa alisema anaunga mkono kuondolewa kwa vizuizi vinavyowakabili wanawake na wasichana kuafikia uwezo wao kamili.

“Tuna ndoto ya nchi ambamo kila mwanamke na msichana anafurahia usawa wa kijinsia; nchi ambamo vizuizi vyote vya kisheria, kijamii na kiuchumi vinavyozuia ustawi wa wanawake na wasichana vimeondolewa.

Mama wa Taifa alisema hayo leo katika kikao maalum cha Kongamano la mwaka 2019 la Dunia kuhusu Jinsia linalofanyika Jijini Kigali, Rwanda ambalo lilihutubiwa na marais Paul Kagame (Rwanda) na Sahle-Work Zewde (Ethiopia)

Hafla hiyo pia ilihutubiwa na Mkewe Rais Jeannette Kagame, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Akinwumi Adesina na Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika Moussa Faki Mahamat.

Kongamano hilo linalofanyika mara mbili kila mwaka na linaloandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya maudhui “kushughulikia changamoto zinazokumba usawa wa kijinsia” linajadili mbinu za kuboresha suluhisho za kifedha katika masuala ya kijinsia kati mbalina  maswala mengine muhimu.

Mama wa Taifa la Kenya alielezea matumaini yake kwamba kongamano hilo litasaidia kuwapa shime wanawake na wasichana ili kuwawezesha kuchangia vyema uafikiaji wa ajenda ya maendeleo ya bara la Afrika.

“Huu ndio moyo wa maono ya Afrika katika kuharakisha uafikiaji wa maendeleo ya kudumu ya kijamii na kiuchumi. Kujitolea kwetu sote katika juhudi za ‘kutowacha yeyote nyuma’ hakika kunafungua ukurasa mpya katika juhudi zetu za kuafikia usawa wa kijinsia,” kasema Mama wa Taifa Margaret Kenyatta.

Alielezea kampeini yake ya kuhamasisha juu afya ya akina mama na watoto kupitia shirika la Beyond Zero akisema kuafikia huduma za afya ya kimsingi, lishe bora na buheri wa afya ni muhimu katika kubadilisha maisha ya raia wa nchi hii.

Mama wa Taifa alisema kupitia kwa utangamano na wanawake nchini Kenya, ameshuhudia tajiriba ya mageuzi ya wanawake wajasiriamali kupitia vyama vya ushirika vya akiba na mikopo na makundi ya wanawake almaarufu chamas.

“Nimeamini kwamba wanawake wangetumia kanuni hizo hizo kushawishi ugavi wa rasilimali kwa usawa ili kuimarisha afya, elimu na maslahi ya kijamiii katika nchi,” kasema Mama wa Taifa.

Alitaja ukosefu wa mikopo, uwakilishi duni katika nafasi za mamlaka, ukosefu wa umiliki wa ardhi yenye rotuba, na kutokuwa na uwezo wa kuamua matumizi ya fedha katika elimu na afya ni baadhi ya vizuizi vya usawa wa kijinsia.

Ili kushughulikia changamoto hizi, Mama wa Taifa alisema serikali ya Kenya ilichukua hatua za kuunga mkono wanawake ikiwepo kubuniwa kwa Hazina ya Biashara kwa Wanawake ambayo imeboresha uwezo wa wanawake wa kupata mtaji wa kufanya biashara.

Alisema serikali ya Kenya pia ilianzisha Mpango wa Kurahisisha Kuafikia Kandarasi za Serikali ambapo asilimia 30 ya kandarasi za serikali zilitengewa biashara zinazomilikiwa na wanawake, vijana na walemavu.

“Kuwapa wanawake uwezo wa kiuchumi kunawaruhusu kushiriki katika uamuzi katika kiwango cha familia. Kuondoa vizuizi hivi vya kifedha kumebadilisha familia na jamii,” kasema Mama wa Taifa.

Mama wa Taifa alisema kwamba sambamba na mipango ya kuwawezesha wanawake, serikali ya Kenya imeweka sera za kitaifa za kuondoa tatizo la nasuri (fistula) na ukeketaji wa wanawake kufikia mwaka wa 2022.

“Wakati wa Kongamano la Idadi ya Watu na Maendeleo almaarufu ICPD25 lilioandaliwa jijini Nairobi wiki chache zilizopita, nilitangaza kujitolea kwangu kutetea kukomeshwa kwa ukeketaji kufikia mwaka wa 2022 na hii leo nakariri msimamo huo,” kasema Mama wa Taifa.

Akizungumza katika ufunguzi rasmi wa kongamano hilo, Rais Kagame alitoa wito wa kubadili mawazo akisema harakati za kutetea usawa wa kijinsia zapaswa kuwa jukumu la kila mtu sio tu barani Afrika lakini kote ulimwenguni.

“Wakati wowote mwamamke anafaidika, kila mtu hufaidika na hakuna anayepata hasara,” kasema Rais Kagame.

Kwa upande wake, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Adesina alielezea hatua ambazo zimechukuliwa na benki hiyo kuongeza uwezo wa wanawake wa kuafikia mikopo kwa masharti mafuu.

 -PSCU