Fred Matiang'i awazomea TangaTanga Kirinyaga, atoa onyo kali

WhatsApp-Image-2019-05-17-at-10.02.38
WhatsApp-Image-2019-05-17-at-10.02.38
Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang'i jana Ijumaa amewakashifu viongozi dhidi ya kutumia ripoti ya BBI kugawanya wakenya katika matabaka ya kikabila.

Akizungumza katika hafla ya kuchanga pesa kaunti ya Kirinyaga, Matiang'i aliwapa msomo mkali wanaoeneza ubuyu kuwa yeye na katibu wake wa kudumu Kibicho wanapanga njama ya kumdhalilisha Ruto.

"Ningependa kuwajulisha wanasiasa ambao wanadai kuwa eti Kibicho anawahangaisha kwamba sisi ni wafanyakazi wa serikali na tunahudumia kila mtu. Hilo ndilo jukumu letu kama tulivyoagizwa na Rais Uhuru Kenyatta," alisema Fred.

 Wanasiasa wanaogemea kundi la TangaTanga wanahoji kuwa waziri wa usalama wa ndani na katibu wake wanahusika katika figisu figisu za utovu wa usalama katika uchaguzi mdogo uliopita wa Kibra.

Katika uchaguzi huo, wanasiasa wa TangaTanga wanahoji kuwa njama ya kumfurusha aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale ilikuwa imepangwa na wahuni wasiojulikana.

Idadi kubwa ya wabunge hao wanahoji kuwa mkutano ulifanyika kati ya Raila , Kibicho na Matiang'i ili kupanga 'ghasia' hizo.

"Mimi na Katibu wangu wa kudumu ni kama pande mbili za shilingi. Iwapo utaanza vita na yeye basi utakabiliana na mimi. Siogopi kusema haya mbele ya umma. Tutazidi kufanya kazi pamoja," alisema Fred.

Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Joseph Ole Lenko , James Ongwae ,mwakilishi wa wanawake Homabay Gladys Wanga, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed na Katibu Karanja Kibicho ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria na kuhutubu katika hafla hiyo.