Mwanaume auawa na simba huku KWS ikitoa tahadhari

Shirika la huduma kwa wanyama pori nchini wanamsaka simba aliyemuua mchungaji wa mifugo katika mbuga ya kitaifa ya Nairobi Jumatatu usiku.

Weldon Kirui mwenye umri wa miaka 18 alitafunwa na mnyama huyo huku wenzake wakimtazama bila usaidizi wowote kwa kuhofia maisha yao.

Mkuu polisi Nairobi Japheth Koome alisema kuwa wafugaji wanane walikuwa wakichunga mifugo kwenye mbuga walipovamiwa na simba wawili.

Hata hivyo Koome alisema kuwa wachungaji  hao walikuwa mbugani bila ruhusa.

Mkuu wa polisi katika kituo cha Langa'ata Elijah Mwangi anasema kuwa mabaki ya mwili wa Kirui yalichukuliwa katika hifadhi ya maiti ya City.

Wafugaji wengine walikamatwa na kuzuiliwa kwa kuchunga mifugo bila ruhusa katika mbuga hatari.

Naye mkuu wa mawasiliano wa KWS Ngugi Gecaga alisema kuwa juhudi za kusaka simba hao hazijafua dafu.

"Mtego wa kunasa simba hao umetegwa lakini haujakamata," Gecaga alisema.

Aidha alisema kuwa kikosi cha maafisa wa KWS wameanzisha juhudi za kuwasaka.

Aliwatahadharisha wananchi kuwa wangalifu sana huku akiwasihi kuwaarifu  maafisa wa KWS endapo watakapo waona.

Afisa moja wa KWS alisema kuwa Kirui alishambuliwa na simba 2 asubuhi. Wenzake wakaokolewa na walinda usalama.

"KWS inasikitikia kifo cha mwanaume aliyeuawa na simba katika upande wa kusini wa mbuga wa Nairobi. Kikosi cha maafisa wetu akiwemo daktari wa mifugo wanasaka simba hao ilia wahamishe kutoka eneo hilo," taarifa kutoka KWS ilisema.