Hisia za kimwili! wanawake wahasiriwa wa mafuriko Kilifi, wataka kondomu

Afisa mmoja wa Afya katika Kaunti ya Kilifi jana alilazimishwa kuondoka kwa ghafla katika mkutano wa umma kutafuta mipira ya kondomu kusambaziwa mamia ya wanawake walioachwa bila makao kutokana na mafuriko ili waweze kujikinga dhidi ya maambukizi ya vurusi vya Ukimwi na maradhi mengine ya zinaa.

Hii ni baada ya baadhi ya wanawake kati ya 2000 wanaoishi katika kambi za muda kutoka Lokesheni ya Garashi, Kaunti ndogo ya Magarini kusisitiza kwamba walikuwa wanakabiliwa na hatari ya kuzidiwa na hamu ya kutaka ngono na kujipata wakishiriki mashambulizi na wanaume wanao wamezea mate katika kambi wanamoishi. Wanasema mahema yao yamesongeana sana na huenda wakashindwa kujidhibiti kwa sababu mabwana wao hawako karibu.

“Kwa vile tumekuwa tukiishi hapa kwa zaidi ya majuma mawili bila mabwana wetu ambao wanafanya kazi mashambani mbali nasi wakitunza mali zetu, tuna hamu zetu za kawaida za kike na huenda tukashawishiwa viurahisi na wanaume ndani ya kambi kushiriki mapenzi nao,“ mmoja wa wanawake hao alimweleza Afisa wa Afya Bwana Amos Nthenge aliyekuwa amezuru eneo hilo kutathmini hali ya afya ndani ya kambi hizo.

Wanawake hao walisisitiza kwamba hawangemsikiza kabla ya kupewa mipira ya kondomu ili wajihami nazo tayari kwa makabiliano ikiwa watajipata katika mtego wa hisia za kimwili.